MABINGWA wa Kombe la Kagame, Yanga wameendelea kuvuna neema, baada ya wabunge mashabiki wa klabu hiyo jijini Dodoma, kukubali kuchanga Sh500,000 kila mmoja ili kusaidia maendeleo. Mbali na ahadi hiyo, pia wachezaji wa Yanga walipozwa na Sh2 milioni zilizochangwa fasta na wabunge hao kama pongezi kwa kutwaa taji hilo. Yanga ilitwaa taji hilo, baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0 katika mchezo wa fainali wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa ni mara ya pili kulitwaa kombe hilo, baada ya mwaka jana kuifunga Simba 1-0 kwenye uwanja huo. Uamuzi wa kuichangia Yanga kila mwaka ulitangazwa juzi jioni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala bora, George Mkuchika ambaye ni mmoja wa wapenzi wa Yanga. Hiyo imekuja siku moja tangu wabunge mashabiki wa Yanga kuzindua rasmi tawi lao mkoani hapa, ambapo Mohamed Misanga aliteuliwa kuwa mwenyekiti na Katibu wake, Geofrey Zambi. Kauli ya Mkuchika aliitoa wakati wa kupata futari na wachezaji wa Yanga, ambao hiyo juzi waliliteka Bunge baada ya kutambulishwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda. Akizungumza baada ya kufuturu na wachezaji hao, Mkuchika alisema wabunge mashabiki wa Yanga wameamua kuchanga Sh500,000 kila mmoja kwa mwaka ili kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri. Ombi la kuwataka wabunge ambao ni wanachama na mashabiki wa Yanga waangalie uwezekano wa kuichangia klabu hiyo liliwasilishwa na mfadhili wa timu hiyo, Fatma Karume. “Baada ya kupata ombi hili kutoka kwa Karume, nimeshaanza kupokea michango kutoka kwa wabunge mbalimbali na michango hii inaendelea,” alisema Mkuchika. Mkuchika alifafanua kuwa kutokana na mapenzi makubwa kwa timu hiyo, mara tu alipomwambia Mbunge wa Kilosa, Mustafa Mkullo, papo hapo alitoa mchango wake. “Humu ndani tunafahamiana, michango hiyo tumeipata kwa haraka na fedha nyingine ndiyo tumetumia kuandaa hii futari…Tungepata muda wa kutosha ingekuwaje?”alihoji Mkuchika. Waziri Mkuchika aliwataka viongozi na wachezaji wa Yanga kuhakikisha wanafanya vizuri na kuiletea klabu hiyo vikombe vingi vya kimataifa na kwamba wapo tayari kuisaidia. Akikabidhi kitita cha Sh2 milioni kwa nahodha wa timu ya Yanga, Nadir Haroub, Mwenyekiti wa Yanga Tawi la Bunge, Misanga alisema fedha hizo ni michango ya wabunge wanachama na mashabiki wa Yanga. Katika futari hiyo, baadhi ya wabunge walijitokeza waziwazi na kusema wao ni mashabiki wa timu hiyo ya Yanga wakiwamo wabunge wa Viti Maalumu Grace Kiwelu wa Chadema na Esther Matiko, Vicky Kamata na Martha Mlata ambao ni wabunge wa Viti Maalumu(CCM). Wabunge wengine Mwigulu Nchemba (Iramba Mashariki), Danstan Kitandula (Mkinga), John Shibuda (Maswa Mashariki) na Asumpta Mshama (Nkenge). SOURCE GAZETI LA MWANAINCHI |
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA AFYA NA UKIMWI YAPONGEZA UTEKELEZAJI WA AFUA
ZA UKIMWI NJOMBE
-
NA. MWANDISHI WETU – LUDEWA
MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI,
Mheshimiwa Dkt. Elibariki Kingu ametoa piongezi kwa Mkoa...
9 hours ago
No comments:
Post a Comment