Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Sunday, August 12, 2012

Mwakyembe asema atamtimua kazi meneja wa TAZARA



WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe amesema kuwa atamfukuza kazi Meneja Mkuu wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA), Abdallah Shekimweri iwapo atashindwa kusimamia majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuwapa vitendea kazi na posho wafanyakazi wa shirika hilo.
Licha ya kusema hayo, ameahidi kutembelea Tazara kesho na pia kukutana na upande wa Zambia ili kujadili matatizo yaliyopo katika reli hiyo na kuyapatia ufumbuzi.
Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam, alipofanya ziara ya kushitukiza kujionea utendaji kazi katika karakana za Tazara, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Bandari.
Dk. Mwakyembe, alisema, haridhishwi na ufanyaji kazi katika karakana ya Tazara na kumtaka Shekimweri kuwapa vifaa wafanyakazi hao na iwapo atashindwa kufanya hivyo, atalazimika kumfukuza kazi.

“Jamani tutafukuzana hapa, vijana wapo tayari kufanya kazi, lakini mnawakwamisha …naomba mmueleze Shekimweri kuwa nitamfukuza na niwahakikishie kuwa ninalazimika kurudi hapa kesho Jumatatu,” alisema Mwakyembe.
Alisema kuwa, anashangazwa kuona menejimenti ya Tazara ikishindwa kutoa fedha kwa watumishi wakati serikali imeshatoa ili kukarabati mabehewa ya treni yanayotakiwa kuanza kutoa huduma ya usafiri kwa wakazi wa jijini kuanzia Oktoba, mwaka huu.
“Hivi naomba niulize hizo fedha mnaziweka makao makuu ni maua hayo…naomba muwalipe watu fedha zao na mnunue vifaa, nawaambia kweli tutafukuzana hapa, hakuna wa kunilaumu,” alisema Mwakyembe.
Hata hivyo, aliitaka menejimenti hiyo kukamilisha mabehewa 14 aliyoyaagiza ambapo hadi sasa ni mabehewa manne ndiyo yaliyoonekana kuanza kukarabatiwa.
Baadhi ya watumishi waliokuwa eneo hilo, walilalamikia hatua ya menejimenti ya Tazara kushindwa kupeleka makato ya mishahara yao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ukiwemo, NSSF.
Pia, walidai kuwa huu ni mwezi wa pili hawajalipwa mishahara yao hatua inayowafanya waishi kwa tabu na familia zao.
Mwakyembe alimtaka meneja wa karakana hiyo kuhakikisha watumishi hao wanalipwa posho zao kwa wakati.
Kwa upande wa TRL, waziri huyo, aliliridhishwa na utendaji kazi na kusema kuwa, anaamini wanaenda na muda na ifikapo Oktoba, huduma ya treni itaanza kama ilivyotangazwa.
Usafiri wa njia ya treni kwa wakazi wa jijini, unatarajia kuanza kutolewa Oktoba mwaka huu kwa lengo la kuondoa tatizo la msongamano.
TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment