Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, August 30, 2012

MWANASIASA MKONGWE HAWA NGULUME AFARIKI DUNIA

Hawa Ngulume afariki dunia Mwanasiasa mkongwe aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Kinondoni, Mbarali na Bagamoyo, Mama Hawa Ngulume amefariki dunia leo asubuhi Jijini Dar es Salaam kwani Mama Hawa Ngulume alikuwa akisumbuliwa na kansa kwa muda mrefu.....Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi, Amina.
Marehemu Mama Hawa Ngulume (kushoto) enzi za uhai wake akiwa na Mzee Kingunge Ngombale Mwiru (kulia)  na John Guninita ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam. 

Taarifa tulizozipata hivi punde ni kuwa aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Kibaha, Bagamoyo na Mbarali kwa vipindi tofauti Bibi Hawa Ngulume amefariki dunia jijini Dar es Salaam leo asubuhi.

Kwa kujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana taratibu za mazishi zinaandaliwa na taarifa kamili itatoilewa baadaye.

Mama Ngulume amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya kansa kwa kipindi kirefu .


wakati huo huo... Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametuma Salamu za Rambirambi kwa Familia ya aliyepata kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Mama Hawa Ngulume kufuatia taarifa za kifo chake kilichotokea katika Hospitali ya Jeshi Lugalo, Jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu akisumbuliwa na ugonjwa wa Saratani. Mama Hawa Ngulume amefariki leo tarehe 30 Agosti, 2012.

Katika Salamu zake hizo, Rais Kikwete amesema Marehemu Hawa Ngulume, enzi za uhai wake, alikuwa kiongozi shupavu aliyesimamia maamuzi yake katika majukumu muhimu ya kitaifa kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo katika sehemu zote alizotumikia akiwa Mtumishi wa Umma, na baadaye alipopewa wadhifa wa Mkuu wa Wilaya alioutumikia katika Wilaya za Singida Mjini katika Mkoa wa Singida, Kinondoni Mkoani Dar es Salaam na mara ya mwisho katika Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya.

“Nilimfahamu Marehemu, enzi za uhai wake, kama Kiongozi Mwanamke shupavu aliyesimamia kikamilifu maamuzi yake, na hivyo kuthibitisha ukweli kwamba wanawake wakipewa fursa wanaweza”, amesema Rais Kikwete katika kuomboleza kifo chake.

“Kutokana na msiba huo mkubwa, natuma Salamu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa Familia ya Marehemu, Mama Hawa Ngulume kwa kuondokewa na Mhimili muhimu na Kiongozi wa Familia. Natambua machungu mliyo nayo hivi sasa kwa kumpoteza Mama wa Familia, lakini nawahakikishia kuwa niko pamoja nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa”, ameongeza kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.

Rais Kikwete amewataka wanafamilia ya Marehemu wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri wakati huu wanapoomboleza msiba wa mpendwa wao kwani yote ni Mapenzi yake Mola. Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu Mama Hawa Ngulume, Amina.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment