Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, September 13, 2012

Morgan Tsvangirai ashinda kesi ya ndoa




Mahakama nchini Zimbabwe imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa mahakamani na mwanamke mmoja kumzuia waziri mkuu wa nchi hiyo Morgan Tsvangirai kufunga ndoa na mpenzi wake Elizabeth Macheka Jumamosi hii.
Locadia Tembo alisema kuwa harusi hiyo haiwezi kufanyika kwani yeye ni mke wa kitamaduni wa Tsvangirai
Rais Robert Mugabe, anatarajiwa kuhudhuria harusi hiyo.Lakini jaji wa mahakama kuu Antonia Guvava alisema kuwa harusi za kitamaduni sio halali tena nchini Zimbabwe.
Mwandishi wa  mjini Harare Brian Hungwe, anasema kuwa harusi hiyo inatarajiwa kufanyika katika mtaa mmoja wa kifahari Kaskazini mwa Harare.
Rais Mugabe pia anatarajiwa kuandaa dhifa ya baada ya harusi ambayo itahudhuriwa na marais walioalikwa kwa harusi hiyo.
Bwana Tsvangirai, mwenye umri wa miaka 59 na rais Mugabe ambao ni viongozi wa muungano wa vyama tawala,
MDC na Zanu-PF wanatarajiwa, kugombea urais kila mmoja kwa chama chake mwaka ujao.
Kesi iliyowasilishwa na Bi Tembo mwenye umri wa miaka 39 dhidi ya Tsvangirai, ilisikilizwa faraghani katika mahakama kuu mjini Harare.
Jaji aliamua kuwa ndoa za kitamaduni sio halali ila ikiwa tu kwa mazingira maalum mfano ikiwa ni kwa misingi ya kugawana mali za wanandoa.
Pia alisema kuwa kesi hiyo ilipaswa kushughulikiwa na afisaa anayehusika na maswala ya ndoa katika mahakama ya hakimu.
Wakili wa Bi Tembo Everson Samkange, alisema kuwa atawasilisha pingamizi zaidi katika mahakama ndogo ambayo itaweza kupelekea kuundwa kwa tume maalum ikiwa kesi itaendelea.

No comments:

Post a Comment