Na Ally Mohamed,
Zanzibar
LIGI Kuu ya
Zanzibar, maarufu Zanzibar Grand Malt Premier League imeendelea tena jana na
kwenye Uwanja wa Amaan, mjini Unguja, Mtende Rangers, ilichomoza na ushindi wa
mabao 3-0 dhidi ya Zimamoto, mabao yake yakitiwa kimiani na Ali Salum dakika ya
tano, Ali Manzi dakika ya 42 na Islah Khamis dakika ya 77.
Katika mechi
za juzi, Uwanja wa Amaan mjini Unguja, Malindi ambao wameinunua timu ya
Miembeni SC, waliteremka uwanjani kuivaa Bandari ambayo imepanda daraja msimu
huu, katika mechi hiyo Bandari wameianza vyema ligi hiyo baada ya kuchomoza na
ushindi wa mabao 3-2. Mabao ya Bandari yalifungwa na Mussa Omar katika dakika
ya 31, Haisam Khamis dakika ya 57 na Shariff Kitwana katika dakika ya 78, wakati
mabao ya Malindi yalifungwa na Amour Suleiman dakika ya 44 na 68.
Huko
kisiwani Pemba, wawakilishi wa Zanzibar katika michuano ya Kombe la Shirikisho
Afrika mwakani, Jamhuri wakicheza na Duma ambayo inamilikiwa na Jeshi la
Kujenga Uchumi (JKU) wameanza vizuri baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao
2-0, yaliyotiwa kimiani na Mfaume Shaaban katika dakika ya saba na 72.
Ligi hiyo
inatarajia kuendelea tena kesho, kwa mchezo mmoja ambao utapigwa Uwanja wa
Amaan ukiwakutanisha Mtende Rangers na Zimamoto mechi itakayoanza saa 10:30
jioni.
Mapema Jumamosi,
pazia la ligi hiyo lilifunguliwa mechi mbili kuchezwa katika viwanja viwili
tofauti, kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja, Mabaharia wa KMKM walikutana
na Mafunzo, ambapo mechi hiyo imemalizika kwa Mafunzo kuchomoza na ushindi wa
bao 1-0, bao hilo pekee likipatikana katika dakika ya tano, mfungaji Mohammed
Abdulrahman.
Huko
kisiwani Pemba nako ilipigwa mechi moja ikiwakutanisha mabingwa watetezi wa
ligi hiyo, Super Falcon na Chipukizi ambapo kwa mara nyengine tena Super Falcon
ambao ni wawakilishi wa Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani,
wamefungwa 2-0.
Hiyo ni
mechi ya sita mfululizo Super Falcon wanapokea kipigo, wakianzia katika
michuano ya BancABC Super 8, ambapo walipoteza mechi zao zote 3 za hatua ya makundi,
kabla ya kukubali kipigo cha 3-1 kutoka kwa Jamhuri katika mechi ya Ngao ya
Jamii iliyochezwa Septemba 1, mwaka huu Uwanja wa Amaan na juzi wakicheza na
Coastal Union ya jijini Tanga katika mechi ya kirafiki, mchezo uliochezwa
Uwanja wa Ngome, Fuoni, Wilaya ya Magharibi, Unguja walifungwa 2-0.
Ligi kuu ya
Zanzibar, ambayo msimu huu inafahamika kwa jina la Zanzibar Grand Malt Premier
League kutokana na mdhamini kinywaji cha Grand Malt, inashirikisha timu 12,
huku timu 8 zikitoka kisiwani Unguja na timu 4 zikitoka kisiwani Pemba, timu
zinazotoka kisiwani Unguja ni Bandari,
Chuoni, KMKM, Mafunzo, Malindi, Mundu ambao wamenunua daraja kutoka kwa
Miembeni United, Mtende iliyopanda daraja msimu huu na Zimamoto. Kwa upande wa
kisiwani Pemba ni Chipukizi, Duma, Jamhuri na Mabinwa watetezi, Super
Falcon. Ligi hiyo inatarajia kuendelea
tena leo kwa mechi moja na ya mwisho katika mzunguko wa kwanza, kwenye Uwanja
wa Amaan, majira ya saa 10:30 jioni kwa kuzikutanisha timu za Chuoni na Mundu.source http://bongostaz.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment