Lile 'jumba' kali la Mchungaji na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mchungaji Dk. Getrude Rwakatare na ambalo lilidaiwa kuzinduliwa kwa mbwembwe hivi karibuni, ni miongoni mwa majumba ya kifahari yanayotakiwa kuvunjwa mara moja kwa madai kwamba yamejengwa kinyume cha sheria za mazingira kwani yote yapo katika maeneo ya kandoni mwa mito ya Mbezi Beach, Mndumbwe na eneo la Hifadhi ya Mikoko jijini Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa salama pekee ya mjengo wa Mama Lwakatare unaokadiriwa kuwa na thamani ya Sh. bilioni 1.5 itategemea maamuzi ya mahakama ambayo hadi sasa ndiyo iliyositisha zoezi la kulivunja.
Jana, Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Manchare Heche, alikaririwa katika taarifa ya gazeti la NIPASHE akithibitisha kuwapo kesi iliyofunguliwa na mmiliki wa jumba hilo katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi na kwamba itatajwa wiki ijayo (Septemba 20, 2012).
Baadhi ya majumba katika maeneo hayo yameshabomolewa katika operesheni ambayo pia ilihusisha Wizara ya Maliasili na Utalii na kusimamiwa na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi la Polisi, Julai 7, mwaka huu, lakini jumba la Mama Lwakatare liliachwa kutokana na kuwapo zuio la mahakama.
You might also like:
No comments:
Post a Comment