MBUNGE wa
Iringa mjini na Waziri Kivuli wa Mali Asili na Utalii (Chadema) Mch.
Peter Msigwa amemtaka rais Kikwete kuchukua hatua za maksudi na
kuingilia kazi za Waziri wa Maliasili na Utalii kwa madai kuwa waziri
huyo ameshindwa kazi na anakula sahani moja na majangili.
Akiongea
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Msigwa amesema
anasikitishwa na hatua ya serikali kukaa kimya ili hali ujangili wa
pembe za ndovu ukiendelea huku waziri huo wa mali asili na utalii Balozi
Hamisi Kagasheki akiwa kimya.
Msigwa
aliyasema hayo kufuatia kukamatwa kwa pembe za ndovu huko Hong Kong,
China jambo ambalo alitegemea Tanzania wizara husika ungechukua hatua za
haraka kubaini wezi waliosafirisha bidhaa hiyo lakini wizara imekaa
kimya hata baada ya mamlaka za China kuomba taarifa za mtandao wa
biashara hiyo.
“Pembe za
ndovu zenye uzito wa tani 4 kutoka nchini Tanzania na Kenya
zimeripotiwa kukamatwa na vyombo vya usalama vya mamlaka ya jiji la Hong
Kong hivi karibuni, huku zile zilizoibwa kutoka Tanzania zikiwa na
thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5 lakini waziri hata hashtuki
amekaa kimya”
Alisema
wizi huo wa pembe za ndovu ni matokea ya waziri Kagasheki kuendelea
kuwalinda watuhumiwa wakuu wa ujangili na kufanya danganya toto kwa
kuwachukulia hatua watuhumiwa watatu tu wadogo, huku wale vigogo wa
ujangili wakiachwa waendeleze ujangili kwa maslahi anayoyajua yeye na
chama chake cha CCM.
“Kuendelea
kwa matukio ya ujangili ni ushahidi kuwa mabadiliko ya Mawaziri
yaliyofanywa na Rais Kikwete kwa kuwatoa Maige na kumweka Kagasheki
hayajazaa matunda yoyote, kwani udhaifu au ufisadi wa Kagasheki hauna
tofauti yoyote ile na ule uliosababishwa na mtangulizi wake
aliyeondolewa” alisema Msingwa.
Akitoa
msimamo wake juu ya jambo hilo waziri huyo kivuli wa mali asili na
utalii amesema wizara ya maliasili na utalii ni njia kubwa ya utoroshaji
na wizi wa rasilimali za taifa na kwamba pamoja na mabadiliko ya
mawaziri bado ufisadi unaendelea.
“Kwa mara
nyingine tena napenda watanzania wafahamu kwamba uwendawazimu ni
kufanya jambo lile lile kwa njia ile ile huku ukitengemea matokeo
tofauti, kwa kadri muda unavyozidi kwenda wanyama pori na rasilimali
nyingi za nchi hii zitaendelea kuibiwa na kuuawa, naomba rais achukue
hatua za maksudi kunusuru hali hii” alisema Msigwa.
Chanzo: tabianchi blog
No comments:
Post a Comment