MATUMIZI
makubwa ya fedha katika uchaguzi ndani ya CCM na Jumuia zake
yanayofanywa na baadhi ya wanachama wasio waaminifu, yameendelea
kulalamikiwa ambapo, kwa sasa mikakati ya kuwadhoofisha wagombea wengine
imebainika.
Miongoni
mwa wagombea wanaodaiwa kuwa wako kwenye mtego wa kudhoofishwa ni Martha
Mlata, ambaye anawania nafasi ya Mwenyekiti wa Wazazi Taifa.
Habari
zilizopatikana zinadai kuwa, baadhi ya vigogo wanaohusishwa na mbio za
urais katika uchaguzi mkuu wa 2015, wametenga fungu kubwa la fedha
kuhakikisha mgombea wao anachukua nafasi hiyo.
Pamoja na Mlata, wanaowania Uenyekiti wa Wazazi Taifa, ni John Barongo na Abdallah Bulembo.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wajumbe walisema kuwa wanachama
wanaotumia fedha kwa ajili ya kupanga safu ya uongozi hawana mapenzi
mema na Chama na kwamba, wamelenga kukitumia kwa maslahi binafsi.
Hata
hivyo, wamesema kuwa kamwe hawatakubali kuona hilo likifanyika na
kwamba, wataingia kwenye chumba cha kupiga kura na kumchagua kiongozi
bora na mwenye mapenzi mema na CCM.
"Mambo
yanayoendelea ni machafu na hatutakubali yapite kama wanavyotaka, CCM ni
ya Watanzania wote hivyo mambo ya watu wachache kupanga safu za uongozi
hatutakubaliana nayo. Wameanza katika uchaguzi ngazi za wilaya, mikoa
na sasa wanakuja taifa kwenye jumuia kuharibu," alisema mwanachama mmoja
ambaye hakupenda kutajwa jina.
Mwana-CCM
huyo alidokeza kuwa, uchaguzi wa UWT uligubikwa na vitendo vichafu na
ukiukwaji wa taratibu ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa ya fedha na
kwamba, hata kuangushwa kwa Martha na Namelok Sokoine kulipangwa mapema.
Martha
alikuwa akichuana na Namelok katika kuwania nafasi ya uwakilishi wa UWT
katika Jumuia ya Wazazi, ambapo nguvu kubwa ya fedha ilitumika
kumwagusha ili kutengeneza mazingira ya kumdhoofisha katika kuwania
nafasi ya Mwenyekiti wa Wazazi Taifa.
Kwa
upande wake Martha alipoulizwa, alisema ni muda mrefu amekuwa akifanyiwa
kampeni chafu kwa lengo la kumwangusha katika harakati zake za kuwania
nafasi hiyo, lakini hatimaye wajumbe ndio watafanya maamuzi.
"Mimi
namwachia Mungu na waamuzi wa mwisho ni wajumbe wa mkutano mkuu wa
Wazazi, kila kukicha nafanyiwa kampeni chafu ili nishindwe. Nia yangu ni
kuitumikia jumuia na CCM na watanzania ili kusukuma gurudumu la
maendeleo, sasa kama wengine wanatumia fedha kuharibu basi viongozi
wataamua la kufanya," alisema Martha.
No comments:
Post a Comment