Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, October 15, 2012

Mauaji ya RPC 15 wakamatwa


SIKU moja baada ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza (RPC), Liberatus Barlow (52), kuuawa na kundi la watu wanaosadikiwa kuwa majambazi, taarifa zinasema polisi wa kimataifa watashirikishwa kufanya uchunguzi na kukamata wahusika wa tukio hilo.

Polisi mkoani Mwanza wameapa kupambana kuwasaka waliohusika katika tukio hilo la kinyama, huku idadi ya watu waliokamatwa hadi kufikia Jumapili jioni ikitajwa kufikia watu 15.


Kamanda Barlow enzi za uhai wake

Taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo zilizopatikana jijini Mwanza zinaeleza kwamba, idadi hiyo ya watuhumiwa waliokamatwa huenda ikaongezeka maradufu kuanzia kesho Jumatatu, baada ya marehemu Barlow (pichani), kuagwa jijini hapa kesho kisha kusafirishwa hadi nyumbani kwake Dar es Salaam, na baadaye Jumanne kusafirishwa nyumbani kwao mkoani Kilimanjaro tayari kwa mazishi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo baadaye Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Lily Matola pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba walikataa kutaja idadi halisi ya watuhumiwa waliowakamata, zinadai kwamba upelelezi wa kina na wa hali ya juu unafanyika kote nchini, ikiwa ni pamoja na maeneo ya mipakani ili kuwanasa watuhumiwa wa mauaji hayo.

“Kazi ya kukamata watu wanaoshukiwa inaendelea. Na hadi leo Jumapili zaidi ya watu 15 wameshakamatwa… na upelelezi wa kina unafanyika kila kona ya nchi hii na hadi maeneo ya mipakani.

“Kuuawa kwa Kamanda Barlow si tukio dogo. Inahitajika nguvu ya ziada kuwanasa watuhumiwa, ndiyo maana IGP Said Mwema amemtuma haraka sana kuja Mwanza DCI Manumba. Ninyi subilieni tu mtasikia…wote waliohusika tutawakamata tu”, kilisema chanzo cha habari kutoka ndani ya jeshi la polisi mkoani Mwanza (jina tunalihifadhi).

Kuhusu ripoti ya madaktari
Alipoulizwa na FikraPevu iwapo uchunguzi wa madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), ya jijini Mwanza juu ya mwili wa marehemu Barlow, Kaimu Kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa, Matola alisema jopo la madaktari bado wanaendelea kufanyakazi yao ya uchunguzi.

“Suala la ripoti ya madaktari kuhusu mwili wa RPC Barlow bado wanaendelea huko hospitalini Bugando. Subilieni tutawaambia tu ndani ya siku chache!”, alisema Kaimu Kamanda huyo wa polisi mkoani hapa, Matola.

Kufuatia taarifa hiyo ya Matola, habari za awali zilizopatikana kutoka kwa vyanzo vyetu Bugando zinadai kwamba, hadi kufikia leo alasiri tayari jopo la madaktari walikuwa wameshamaliza uchunguzi wao juu ya marehemu Kamanda wa polisi mkoani hapa.

Inadaiwa kwamba, miongoni mwa risasi zilizompata kamanda huyo, risasi moja ilimpiga shingoni kisha kuvunja na kuharibu kabisa shingo pamoja na mfumo wa damu, hali iliyosababisha kuvuja kwa damu nyingi.

Makachero wa Interpol kusaidia
Inadaiwa kwamba ili kufanikiwa kuwanasa watuhumiwa wa mauaji hayo ya RPC Barlow, jeshi la polisi limeomba ushirikiano kutoka Kitengo cha upelelezi cha Interpol.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini Mwanza, zinadai kwamba baadhi ya askari kutoka vikosi hivyo vya Interpol hapa nchini na nchi jirani vimeshaanza kuwasili kisha kusambaa katika maeneo tofauti Ukanda wa nchi zote za Maziwa Makuu, na kwamba watuhumiwa wote lazima wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

“Polisi imeshaomba msaada wa kikosi cha Interpol ili kusaidia kuwanasa wauaji hawa. Hapana shaka lazima watu waliohusika kummiminia risasi na kupoteza uhai wa RPC Barlow watakamatwa tu. Achana na kazi ya Interpol, maana hata mtu amejificha kwenye handaki atapatikana tu”, kilisema chanzo kingine cha habari.

Katika hilo, Kaimu Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Matola alipoulizwa na FikraPevu iwapo ni kweli wameomba msaada na nguvu ya kiupelelezi kutoka kwa askari wa Interpol, alishindwa kukubali wala kukanusha, bali alisema:

“Naomba mambo mengine mtuachie sisi, maana bado tunaendelea kufanyakazi hii ya upelelezi. Na tunachokiamini ni kwamba wahusika wote wa mauaji ya RPC Barlow lazima wakamatwe”.

Aidha, Kamanda Matola aliwaomba wananchi wote kulisaidia jeshi hilo la polisi katika kuwabaini wahusika wakubwa wa tukio hilo la kuuawa kwa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, na kwamba waandishi wa habari nao ni sehemu na nguzo muhimu katika kulisaidia jeshi hilo kufikia malengo yake ya kupambana na wahalifu ndani na nje ya mkoa huo.

DCI Manumba anena
Katika mahojiano yake na mwandishi wa habari hizi jioni hii, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba alisema kazi inayofanywa na jeshi hilo la Polisi lazima itawanasa watuhumiwa wote wa mauaji hayo.

“Nina uhakika wahusika wote wa mauaji ya Kamanda Barlow tutawakamata. Kwa sasa kazi ya upelelezi bado inaendelea kufanyika, lakini tutahakikisha sheria inachukuwa mkondo wake kwa watuhumiwa wote”, alisema DCI Manumba kwa njia ya simu yake ya kiganjani.

Alipotakiwa kutaja idadi ya watu waliokwisha kukamatwa tangu mauaji ya Kamanda huyo wa Polisi mkoani Mwanza, DCI Manumba ambaye amejichimbia jijini hapa kwa lengo la kuongeza nguvu ya kiupelelezi alisema:

“Hilo la idadi siwezi kusema. Naomba mtuache kwanza tutawaambia mara baada ya kazi kukamilika. Vuteni subira, kazi bado inafanyika”.

No comments:

Post a Comment