WINGU
la rushwa limeendelea kutanda katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), na sasa
Mbunge wake wa Ilala, Mussa Zungu, anashilikiwa na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), akituhumiwa kutoa rushwa kwa baadhi ya
wajumbe wa Jumuiya ya Wazazi.
Zungu
ambaye anakuwa mbunge wa pili wa CCM kunaswa na TAKUKURU kwa tuhuma za
rushwa, anashikiliwa pamoja na wajumbe wawili wa jumuiya hiyo.
Mbunge
huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge, alikuwa akigombea nafasi ya
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) kupitia Jumuiya
ya Wazazi Tanzania Bara na alinaswa juzi sambamba na Dk. Damas Mukasa na
Fatuma Kasenga.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa
Dodoma, Yunis Munisi, alisema Zungu alikamatwa Oktoba 30, mwaka
huu, siku moja kabla ya uchaguzi huo.
Akielezea
mazingira ya kukamatwa kwao, alisema Zungu alikamatwa akiwa na wapambe
wake wanne akitoa rushwa kwa wajumbe ili wampigie kura.
Kuhusu
Dk. Mukasa ambaye alikuwa akigombea nafasi ya ujumbe wa Baraza Kuu la
Wazazi Taifa na mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM Taifa, Munisi alisema
alikamatwa Oktoba 8, mwaka huu, nje ya Ukumbi wa Kilimani mjini hapa kwa
kosa la kutoa rushwa kwa wajumbe ili wampigie kura.
Pamoja
na hilo, wajumbe wengine wawili nao wanashikiliwa na TAKUKURU kwa kosa
la kupokea rushwa kutoka kwa Dk. Mukasa ili wamchague.
Mgombea
mwingine aliyekamatwa, Fatuma, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazazi Mkoa wa Mbeya na Mkutano Mkuu Wazazi Taifa, alikamatwa saa tisa
usiku wa kuamkia jana akiwa analipia baadhi ya wajumbe wa mkutano
vyakula na vinywaji.
“Inaaminika
kwamba huo ulikuwa ni ushawishi ili wajumbe wamchague...alikamatwa
katika nyumba ya wageni ya Kitoli iliyopo eneo la Iringa Road mjini
Dodoma,” alisema Munisi.
Alisema
TAKUKURU imekuwa ikifuatilia taarifa za vitendo vya rushwa tangu kuanza
kwa chaguzi za ndani za CCM kuanzia ngazi za chini hadi taifa kwa lengo
la kuzuia na kupambana na vitendo hivyo.
Munisi
alisema hatua hiyo imefanikiwa kuzuia vitendo vingi ambavyo vilitaka
kutendeka baada ya kupata mipango hiyo na kuitibua kabla ya kufanikiwa.
Hata
hivyo, alisema changamoto kubwa waliyokumbana nayo ni kitendo cha
wajumbe kushirikiana na wagombea na wapambe wao katika vitendo vya
rushwa, na hivyo kuwa shida kufanya ushirikiano.
Alisema
changamoto nyingine inatokana na wananchi kudai wameona vitendo vya
rushwa vikitendeka, lakini hawachukui hatua zozote za kutoa taarifa
TAKUKURU.
Kuhusu tuhuma zinazowakabili akina Zungu na wenzake, alisema uchunguzi unaendelea.
Kambi ya Lowassa kidedea
Kambi
inayoungwa mkono na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, imezidi
kuonesha umwamba wake ndani ya CCM kwa kuibuka kidedea katika uchaguzi
wa Jumuiya ya Wazazi uliofanyika jana.
Abdallah
Bulembo ndiye ameibuka mshindi wa nafasi ya mwenyekiti wa jumuiya hiyo
kwa kura 677 na kuwatimulia vumbi washindani wake, Martha Mlata
aliyepata kura 146 na John Barongo aliyeshika nafasi ya mwisho kwa
kuambulia kura 43.
Mapema
akifungua mkutano huo wa uchaguzi, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib
Bilal, aliitaka jumuiya hiyo kuchagua viongozi watakaoweza kukiepusha
chama na rushwa kwa kipindi chao cha miaka mitano.
“Kiongozi
anayehonga ili aweze kupata madaraka huyo si kiongozi na hafahi
kuchaguliwa,” alisema Dk. Bilal na kuwataka wagombea wote kuachana na
imani ya kutumia fedha kutafuta uongozi.
Aidha, makamu huyo aliwataka wazazi kuwa mstari wa mbele katika kuwalea vijana ili maadili yaliyopotea yarudi kama hapo awali.
Dk.
Bilal alisema kuwa wazazi ndio wenye jukumu kubwa la kuwalea vijana na
kuwaongoza katika maadili mema, hivyo ni jukumu lao kubwa kuhakikisha
vijana wanakuwa na tabia njema.
na tanzania daima.
No comments:
Post a Comment