Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, October 27, 2012

NI PATASHIKA SIMBA NA AZAM TAIFA LEO, YANGA KUJIULIZA NA JKT OLJORO


Azam FC


LIGI Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea leo kwa nyasi za viwanja vitano kuwaka moto, huku macho na masikio ya wengi yakiwa katika Viwanja vya Taifa, Dar es Salaam ambako Simba na Azam FC zitakuwa zikimenyana na Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, ambako Yanga SC watakuwa wageni wa JKT Oljoro.
Lakini mechi kali zaidi itakuwa kati ya Azam na Simba ambazo zitagombea usukani wa ligi hiyo, zikiendeleza upinzani wao wa tangu msimu uliopita zilipogombea ubingwa.
Simba ndio inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 19 wakati Azam FC ina pointi 18 na Yanga yenye pointi 14, inashika nafasi ya tatu.
Dhahiri Azam ikishinda leo itapanda kileleni na hali itakuwa mbaya zaidi kwa Simba iwapo na Yanga itashinda, kwani mabingwa hao watetezi watakuwa wanawazidi wapinzani wao wa jadi kwa pointi mbili tu.
Azam ipo kambini kwake Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ilipokuwa ikijifua vikali chini ya kocha wake Mserbia, Boris Bunjak, wakati Simba SC waliweka kambi visiwani Zanzibar tangu Jumanne kujiandaa na mechi ya leo.
Simba iliyokuwa bingwa msimu uliopita na Azam iliyoshika nafasi ya pili, ndizo timu pekee ambazo hadi sasa hazijafungwa hata mechi moja katika Ligi Kuu.
Simba imetoa sare nne, dhidi ya Yanga (1-1), Coastal Union na Mgambo (zote 0-0) na Kagera Sugar (2-2) wakati Azam imetoa sare tatu, 2-2 na Toto Africans, 0-0 na Prisons na 1-1 na Ruvu Shoting.
Mechi ya leo itakuwa kipimo kingine cha kocha Mserbia wa Azam, Bunjak ambaye hadi sasa amekwishaiongoza timu hiyo katika mechi 15 tangu awasili nchini kurithi mikoba ya Muingereza, Stewart Hall, Agosti mwaka huu kati ya hizo akiwa ameshinda tisa, sare tatu na kufungwa tatu.
Mechi zote alizofungwa ni dhidi ya Simba, 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R, 3-2 kwenye Ngao ya Jamii na 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliopigwa Chamazi.
Hivyo leo Bunjak atakuwa na wajibu wa kuwaridhisha matajiri wenye asili ya Kiarabu, wanaoimiliki timu hiyo, kwamba yeye si mnyonge kwa Mserbia mwenzake anayeinoa Simba SC, Profesa Milovan Cirkovick.
Simba baada ya sare ya tatu mfululizo ikaamua kwenda kuweka kambi Zanzibar kujiandaa na mechi ya leo na kwa kawaida Wekundu wa Msimbazi wamekuwa wakienda visiwani humo katikati ya Ligi kuweka kambi, wanapokuwa wanajiandaa na mechi dhidi ya mahasimu wao tu, Yanga.
Kitendo cha kwenda Zanzibar kinamaanisha Simba wanaupa uzito mkubwa mchezo huo wa leo- sawa tu na mchezo dhidi ya Yanga.
Lakini pia kambi ya Simba imekumbwa na mtikisiko kidogo kuelekea mechi hii, kiasi cha kuwasimamisha wachezaji wake wawili beki Juma Nyosso aliyeambiwa afanye mazoezi ni kikosi cha pili ili kuboresha kiwango chake na kiungo Haruna Moshi ‘Boban’, ambaye amesimamishwa kwa wiki tatu kwa utovu wa nidhamu.
Pamoja na hayo, bado kuna wachezaji ndani ya Simba wanaangaliwa kwa jicho la tatu juu ya mwenendo wao, wakiwemo beki Amir Maftah, viungo Ramadhan Chombo, Mwinyi Kazimoto na Mrisho Ngassa.
Safu ya ulinzi ya Simba itakuwa tena na beki wake chipukizi mahiri, Shomary Kapombe ambaye amekosa mechi mbili zilizopita kutokana na maumivu ya kifundo cha mguu na leo anaweza akacheza pamoja na Hassan Kondo katika beki ya kati.
Hayatarajiwi mabadiliko makubwa sana kwenye kikosi cha Simba leo, Juma Kaseja akiendelea kusimama langoni, kulia Nassor Masoud ‘Chollo’, kushoto Amir Maftah, katikati Kapombe na Kondo, kiungo mkabaji Amri Kiemba, kulia Mrisho Ngassa, katikati Mwinyi Kazimoto, kushoto Emmanuel Okwi na washambuliaji Felix Sunzu anaweza akaanza na kinda Christopher Edward leo.
Azam bila shaka Mwadini Ali atasimama langoni, kulia Ibrahim Shikanda, kushoto Erasto Nyoni, katikati Said Mourad na Aggrey Morris, kiungo mkabaji Abdulhalim Humud, kulia Kipre Tcheche, kushoto Kipre Balou, katikati Salum Abubakar na washambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ na Abdi Kassim ‘Babbi’.
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Yanga haitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa sana katika kikosi chake kutoka kile kilichoshinda 3-0 dhidi ya Polisi katika mchezo uliopita.
Ally Mustafa ‘Barthez’ anaweza kuendelea kusimama langoni, kulia Juma Abdul, kushoto Oscar Joshua, katikati Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Mbuyu Twite, kiungo mkabaji Athumani Iddi ‘Chuji’, kulia Simon Msuva, kushoto David Luhende, katikati Haruna Niyonzima na washambuliaji Didier Kavumbangu na Jerry Tegete.
JKT Oljoro; Shaibu Issa, Yussuf Nachogote, Nafo Zuberi au Jackson Semfukwe, Salim Mbonde, Marcus Raphael (Nahodha), Emanuel Memba, Karage Gunda, Saleh Iddi au Amir Omar, Paul Nonga, Meshack Nyambele na Sixbert Mohamed au Essau Sanu.
Mechi nyingine za ligi hiyo leo ni kati ya African Lyon na Kagera Sugar Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, Mgambo JKT na Prisons Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting dhidi ya Polisi Morogoro Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa michezo miwili kati ya JKT Ruvu na Coastal Union Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam na Toto Africans dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Simba SC
REKODI YA SIMBA NA AZAM LIGI KUU:
Februari 11, 2012
Simba SC 2 - 0 Azam FC
Sept 11, 2011
Azam FC 0 - 0 Simba SC
Jan 23, 2011    
Simba 2-3 Azam (Dar).              
Sep 11, 2010
Azam 1-2 Simba (Tanga).
Machi 14, 2010
Azam 0-2 Simba (Dar) 
Okt 24, 2009
Simba 1-0 Azam (Dar)         
Machi 30, 2009
Azam 0-3 Simba (Dar)  
Okt 4, 2008
Simba 0-2 Azam 
Yanga SC
YANGA NA OLJORO MSIMU ULIOPITA:
Aprili 25, 2012
JKT Oljoro 1 – 4 Yanga
Oktoba 23, 2011
Yanga 1 – 0 JKT Oljoro  
JKT Oljoro

No comments:

Post a Comment