Baadhi ya wafanyabiashara wa bodaboda mjini Singida,wakiwa wanasubiri Petrol.

Uhaba mkubwa wa mafuta ulioikumba manispaa ya Singida,umechangia bei ya petrol kupanda kutoka shilingi 2.085 kwa lita moja,  hadi shilingi 6,000.
Uhaba huo ambao umedumu kwa zaidi ya wiki mbili sasa,umeathiri mambo mengi ikiwemo maadhimisho ya kilele cha shehere ya Idd Alhaj kilichofanyika (26/10/2012).
Inadaiwa kuwa wamiliki wengi wa vituo vya kuuzia mafuta mjini Singida wako kwenye mgomo baridi wa kutouza mafuta wakisubiri bei ipande kwanza.
“Kwa kweli kwa sasa tunateseka mno.Utaambiwa kituo  fulani cha  mafuta  kinauza mafuta,ukienda utasikia kuwa wauza mafuta wamewauzia watu wao na hawataki kuuza tena .Vituo karibu vyote kwa sasa vina utaratibu unaofanana kitendo kinachoonyesha dhahiri kuwa zoezi hili limepangwa”,alisema Juma Kidimanda dereva wa bodaboda na kuongeza;
“Sasa hivi kumejitokeza  biashara ya kuuza mafuta ya petrol na dizeli kwenye madumu.Wafanyabiashara hawa wanauza mafuta kwa bei ya juu mno.Nenda pale peoples klabu,utakuta madumu yamepangana na kiuliza bei ya lita moja ya petrol,utaambiwa lita moja ni shilingi 6,000.Kwa bei hiyo,utafanyaje biashara hii ambayo wateja wengi ni wale wa kipato cha chini”.
Kidimanda alisema kuwa biashara yao sasa imekuwa sio ya uhakika kutokana na uhaba huo wa mafuta na kwamba inasababisha kupoteza wateja wao wa kudumu.
Naye Ramadhani Hamisi mfanyabiashara ya bodaboda,amedai  kuwa vituo vichache ambavyo vinatoa mafuta tena kwa muda mfupi,vimekuwa vikipendelea wafanyakazi wa serikali na watu wenye kipato cha juu.
“Mimi naiomba serikali ya mkoa,iingilie kati hali hii,vinginevyo maisha ya baadhi ya wakazi wake maisha yao yatakuwa magumu mno”alisema.
Baadhi ya wauza mafuta wa vituo mbalimbali waliohojiwa na mwandishi wa habari hii,wote walikuwa na jibu fupi linalofafana nalo ni “hakuna mafuta”.Lakini haichukui muda mrefu utasikia kituo hicho kimeanza kuuza mafuta.Ukirudi,unakuta huduma hiyo imesitishwa.Sababu ni kwamba lengo lilikuwa ni kuuza mafuta kwa mtu wao.
Habari zaidi zilizoenea mjini Singida,ni kwamba wamiliki wa vituo hivyo,wanasubiri hadi wiki ijayo ambapo inadaiwa bei ya mafuta itakapopanda.
Wakati huo huo,mkuu wa wilaya ya Singida mwalimu Queen Mlozi,alisema kuwa siku mbili zilizopita,alifanya ukaguzi kwenye vituo vya mafuta akiwa anaongozana na mkurugenzi wa manispaa,walikuta vituo karibu vyote havikuwa na mafuta.
“Baadhi ya wamiliki wa vituo akiwemo Velarian Kimambo,walinihakikishia kuwa magari yao ya kubebea mafuta yako Dar-es-salaam kwa muda sasa yakisubiri kupakia.Kwa kweli nikiri tu kwamba hali ya mafuta ya petrol na dizeli kwenye wilaya yangu,ni ngumu,ngumu mno.Hivi sasa natoka tena na mkurugenzi kwenda kukagua hali ya mafuta ikiwemo kuwanasa watu wanaouza mafuta kwa bei haramu”,alisema dc Mlozi.