Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi (Katikati) akiwakabidhi Mkuu wa Wilaya ya Bahi Betty Mkwasa (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo Ernest msaada wa unga wa mahindi kwa ajili ya watu waliokumbwa na maafa yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha Novemba 1, 2012.
TAARIFA YA MAAFA YALIYOTOKEA KATIKA KIJIJI CHA MSISI TARAFA YA MUNDEMU WILAYA YA BAHI
Mnamo tarehe 1 Novemba, 2012 yalitokea maafa yaliyosababishwa na Mvua zilizonyesha siku hiyo. Maafa hayo yaliyotokea ni pamoja na mtoto mmoja kupoteza maisha halikadhalika uharibifu wa mali za wananchi, taasisi za kiserikali na za dini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Maafa ya Wilaya ya Bahi iliyotolewa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Betty Mkwasa, tathmini ya awali inaonesha watu wapatao 300 hawana mahali pa kuishi na mtoto mmoja wa miaka minne (4) aliyejulikana kwa jina la Neema Lupembe amekufa maji.
Mvua hizo zilisababisha jumla ya kaya sitini (60) nyumba zake kuezuliwa mapaa; makanisa matatu (3), zahanati moja (1) madarasa mawili (2) na ofisi ya CCM ya Kata navyo viliezuliwa. Kufuatia hali hiyo serikali ya Mkoa na Wilaya ya Bahi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamejipanga kutoa msaada kwa waathirika wa maafa hayo.
Jitihada hizo ni pamoja na:
• Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma imetoa mifuko 24 ya unga ya kilo 25 kila mmoja.
• Serikali ya Wilaya itapeleka chakula cha siku saba ambacho ni pamoja na Unga, maharage na mafuta ya kupikia lita 18.
• Chama cha Mapinduzi Mkoa wametoa mifuko 10 ya unga ya kilo 25 kila mmoja. • Chama cha Msalaba Mwekundu kinapeleka mahema na mablanketi kwa ajili ya kaya 34 ambazo ndizo zimeathiriwa vibaya sana.
Ili kuendelea kutoa msaada zaidi kwa watu waliokumbwa na maafa hayo, Kamati mbalimbali zimeshajipanga kuwahudumia waliokumbwa na maafa ikiwa ni pamoja na kamati ya Afya ya Wilaya na tayari Kamati ya Maafa ya Wilaya Bahi imeomba kuuziwa chakula cha bei nafuu kutoka katika ghala la hifadhi ya chakula la Taifa kiasi cha kilo 1622.
No comments:
Post a Comment