Hoteli
ya Kitalii iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam, yenye hadhi ya nyota
tano imeumbuka baada ya kubainika kumwaga maji ya chooni baharini.
Madudu
ya hoteli hiyo inayotambuka kama Double Tree by Hilton, yamebainika
baada ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu
wa Rais (Mazingira), Charles Kitwanga, pamoja na maofisa waandamizi
kutoka Baraza la Taifa la Mazingira (Nemc).
Ziara
hiyo imebaini kwamba mfumo wa majitaka ya hoteli hiyo haujajengwa
vizuri kuruhusu maji hayo kusafishwa kabla hayajamwagwa au kuingizwa
kwenye mfumo wa Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco).
Kitwanga
na maofisa hao wa Nemc walifika kwenye hoteli hiyo majira ya saa 7:00
mchana na kuhoji mfumo wa majitaka pamoja na sababu za hoteli hiyo
kujengwa hadi baharini.
Mameneja
wa hoteli hiyo walimweleza Naibu Waziri kwamba maji hayo yanahifadhiwa
vyema na kisha kuzolewa kwa magari ambayo huenda kuyamwaga kwenye
mabwawa ya majitaka.
Hata
hivyo, Kitwanga alihoji linapopita gari la kuja kuchukua maji hayo kwa
kuwa eneo zima limezungukwa na majengo pamoja na ukuta usioruhusu gari
kupita.
Baada ya kuendelea kukagua, ndipo ilibainika kwamba uchafu wote wa hoteli hiyo na hasa maji ya chooni yanamwagwa baharini.
"Tulichoona
hapa ni kinyesi kabisa, harufu ya maji ya chooni inatoka halafu hawa
wanatudanganya eti ni mtiririko wa maji wa kawaida, hali hii
haikubaliki," alisema Kitwanga.
Kitwanga
alisema serikali inawahamasisha wawekezaji waje kuwekeza nchini, lakini
kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, vinginevyo itawachukulia hatua
stahiki.
Alimweleza
Mkurugenzi Mkuu wa hoteli hiyo, Sven Lippinghof, kwamba kumwaga kinyesi
baharini ni suala lisilovumilika na kumtaka kuzingatia sheria ya
mazingira na nyinginezo ili kulinda afya ya viumbe wa baharini na za
wananchi.
Naibu
Waziri huyo aliitaka Nemc kufuatilia kwa kina usitishwaji wa kumwaga
maji hayo na kumpa mwekezaji huyo wiki moja kwamba hadi Ijumaa ijayo awe
amefanya marekebisho ya kina.
Kwa
upande wake, Mwanasheria wa Nemc, Manchere Heche, aliitaka hoteli hiyo
kusitisha kumwaga maji hayo baharini kuanzia jana na kumwandikia barua
ya kusisitiza amri hiyo.
Alisema kuanzia leo, Nemc itafanya ukaguzi katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba agizo hilo linatimizwa.
"Napenda
tu nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri kwamba suala la afya ya wananchi ni
la msingi na muhimu, leo hii (jana) kwamba Nemc inawataka msitishe
kumwaga haya maji na nitawaandikia barua leo kusisitiza hili," alisema
Heche.
Alisema: "Afya za watu haziwezi kusubiri muda, na tutawatoza faini kwa uchafuzi huu wa mazingira."
Kwa upande wake, Lippinghof alisema atatekeleza maagizo hayo ya Nemc na kwamba suala la kuzingatia sheria halina mjadala.
Alisema atawasilisha pia maagizo hayo kwenye kikao cha bodi ya wakurugenzi wa hoteli hiyo kwa hatua kubwa zaidi.
Awali, ziara hiyo ilifanyika pia kwenye hoteli ya Giraffe ambayo ilibainika kuchafua bahari na kuagizwa kufanya usafi kila siku.
Kadhalika,
Waziri Kitwanga aliiagiza Nemc kusimamisha ujenzi wa hoteli ya Blue
Pearl inayojengwa karibu na Giraffe kwa kuwa imejenga ukuta baharini na
hivyo kuinyima bahari kupumua.
Katika
ziara hiyo, kiwanda cha Coca cola Kwanza ndicho pekee kilichoonekana
kuzingatia sheria ya mazingira kwa kujenga mfumo wa kusafisha maji yenye
sumu kabla hakijayamwaga.
Maeneo
mengine ambayo yalitembelewa na Naibu Waziri huyo ni kiwanda cha dawa
Sheyls Pharmacetical, hoteli za Whitesands na Corol Beach ambazo
zilipewa maelekezo madogo baada ya kubainika kutotimiza masharti ya
sheria ya mazingira.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment