ALIYEKUWA
Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbles Lema, amewasilisha sababu 18,
kuiomba Mahakama ya Rufaa nchini, itengue hukumu ya awali iliyotolewa
na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili mwaka huu ambayo ilifuta ubunge
wake.

Ombi hilo
liliwasilishwa mahakamani hapo jana na mawakili wa Lema, Method
Kimomogoro na Tundu Lissu ambao walidai kuwa hukumu hiyo iliyotolewa na
Jaji Gabriel Rwakibalila haina hadhi ya kuitwa hukumu.
Mbele ya
jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa linaloongozwa na Jaji
Natharia Salum Massati, wakili Kimomogoro, alieleza mahakama kuwa rufaa
ya mteja wake ina jumla ya sababu 18 za kupinga hukumu iliyotolewa na
Jaji Rwakibalila.
Katika
hukumu yake iliyoibua mjadala mkubwa nchini Aprili mwaka huu, Jaji
Rwakibalila alimtia hatiani Lema kwa makosa ya kutoa lugha za kumkashifu
mgombea mwenzie, Dk. Batilda Buriani (CCM) na kumfungia kutogombea
ubunge kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.
Alidai
kuwa, Jaji Rwakibalila alijielekeza vibaya katika hukumu yake alivyosema
kuwa kesi za uchaguzi hazitawaliwi na kanuni za sheria za Uingereza
kwani kuna maamuzi ya kesi mbalimbali yaliyokwishatolewa na Mahakama ya
Rufaa na Mahakama Kuu nchini na kuruhusu kesi za uchaguzi ziamuliwe kwa
kutumia kanuni na sheria za Uingereza.
Katika
hoja ya pili, Kimomogoro alidai kuwa Jaji Rwakibalila alijielekeza
vibaya kuruhusu wajibu rufaa, wasitaje maneno kwenye hati ya madai
ambayo walidai ni maneno ya udhalilishaji wa kijinsia na dini ambayo
yanadaiwa kutolewa na Lema, kwenye mikutano ya kampeni dhidi ya Dk.
Burian.
Hoja
nyingine ni kwamba hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kwamba wajibu
rufaa kama kweli waliandikishwa kupiga kura katika Jimbo la Arusha Mjini
mwaka 2010 au la.
Kwa
mujibu wa wakili huyo, hoja nyingine ni kwamba Jaji Rwakibalila alikosea
kisheria kusema kuwa mtu yeyote akiwemo mpiga kura ana haki ya kufungua
kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo ambalo yeye ni mpiga kura
na kuongeza kuwa, wao wanaomba Mahakama ya Rufaa itamke kuwa wajibu
rufaa (wapiga kura wa Jimbo la Arusha waliofungua kesi ile), hawana haki
kisheria kufungua kesi ile ya kupinga ubunge wa Lema kwani mwenye haki
ya kufanya hivyo ni Dk. Batilda mwenyewe.
Aliongeza kuwa, mpiga kura yeyote hana haki ya kufungua kesi ya kupinga ubunge wa Arusha Mjini kwani haki zao hazikuvunjwa.
Aidha,
katika hoja nyingine alidai kuwa Jaji Rwakibalila hakutumia maamuzi ya
kesi za Mahakama ya Rufaa wala vifungu vya sheria ambavyo mawakili wa
pande zote mbili waliziwasilisha mbele yake katika majumuisho yao ya
mwisho.
Alidai
kuwa, maamuzi ya Mahakama ya Rufaa katika kesi zile yalisisitiza kuwa
lazima kesi ithibitishwe bila kuacha mashaka yoyote, lakini katika
hukumu ya Lema, Jaji Rwakibalila imeacha mashaka mengi, ndiyo maana Lema
anadai jaji huyo alikosea.
Baada ya
wakili Kimomogoro kuwasilisha hoja hiyo iliyodai Jaji Rwakibalila
hakutumia maamuzi ya kesi zilizowasilishwa mbele yake na mawakili wa
pande mbili, Jaji Massati alisema si lazima jaji au hakimu atumie kesi
zilizowasilishwa mbele yake na mawakili katika kutoa uamuzi.
Hoja
nyingine ni kwamba, hukumu ya Lema iliegemea katika ushahidi wa mdomo tu
bila kuwepo ushahidi wa kuunga mkono kwani mashahidi wa mjibu rufaa,
waliotoa ushahidi walidai walimsikia Lema katika mikutano ya kampeni
akitoa maneno ya kumdhalilisha na kumkashfu Dk. Batilda, lakini
walishindwa kuleta CD, mikanda ya video kuthibitisha.
“Tulimueleza
Jaji Rwakibalila kuwa mashahidi wa wajibu rufaa hawaaminiki na kwamba
ushahidi wao ulikuwa wa mazingira, lakini jaji katika hukumu yake hakuna
sehemu aliyoonyesha kukubali wala kukataa hoja yetu hii,” alidai wakili
Kimomogoro.
Wakili
huyo alidai pia Jaji Rwakibalila alikosea alivyosema Lema ana bahati
kwani hakukamatwa wala kushitakiwa kwa kutoa lugha za kashfa na
udhalilisha katika mikutano ya kampeni za uchaguzi wa mwaka 2010.
Kutokana
na madai hayo, alidai kuwa Lema anaiomba Mahakama ya Rufaa itamke kuwa
Jaji Rwakibalila alitamka neno hilo kwa bahati mbaya na kutamka kwake
neno hilo ndiko kulikomsukuma kufikia uamuzi wa kumfungia Lema asigombee
kwa kipindi cha miaka mitano.
“Kwa hoja
hizo tulizoziwasilisha hapo juu, tunaiomba Mahakama ya Rufani nchini
itengue hukumu ya Jaji Rwakibalila kwani haina vigezo wala hadhi ya
kuifanya iwe hukumu, na pia tunaiomba mahakama iwaamuru wajibu rufaa
walipe gharama za uendeshaji wa kesi hiyo tangu ilipoanza Mahakama Kuu
Kanda ya Arusha na sasa Mahakama ya Rufaa,” alidai wakili Kimomogoro.
Kwa
upande wake wakili wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa
Uchaguzi Jimbo la Uchaguzi, Timon Vitalis, alidai kuwa sheria ya
uchaguzi haiwaruhusu wapiga kura kufungua kesi ya kupinga ubunge wala
wagombea ubunge, udiwani kwani aliyepaswa kufungua kesi hiyo ni Dk.
Batilda na siyo wajibu rufaa ambao ni wapiga kura wa Jimbo la Arusha
Mjini.
Hata
hivyo hoja hizo zilipanguliwa na mawakili wa wajibu rufaa, Aluthe Mugwai
na Modest Akida na Wakili wa Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Vitalis.
Mugwai na
Akida walitetea kuwa hukumu ile ni sahihi na haistahili kutenguliwa
kwani imekidhi matakwa ya kisheria na kuomba mahakama hiyo itupilie
mbali rufaa ya Lema.
Mugwai
alisema mawakili wa Lema wanaipotosha mahakama kwa kusema hakukuwa na
uthibitisho wowote ulioonyesha wajibu rufaa walikuwa wapiga kura wa
Jimbo la Arusha Mjini wakati ukurasa wa 10 katika hukumu inayopingwa,
inaonyesha namba za vitambulisho vya wapiga kura ambavyo ni vya wajibu
rufaa na wakati vikitolewa mahakamani, mawakili hao wa Lema walikuwepo.
Kuhusu
hoja ya jaji kwamba alijielekeza vibaya kusema kuwa sheria za Uingereza
hazitakiwi kutumika kuamua katika kesi za uchaguzi, Mugwai alidai Jaji
Rwakibalila yupo sahihi kwani hata kifungu cha 1(2) cha sheria ya
uchaguzi sura ya 343, kinasema masuala yote ya uchaguzi yatashughulikiwa
kwa kutumia sheria ya uchaguzi na kuongeza kuwa mawakili wa Lema
wametumia kesi za Mahakama ya Rufaa zilizoamriwa kwa sheria ya zamani ya
uchaguzi ya mwaka 1985 wakati sheria hiyo ya uchaguzi imeishafanyiwa
marekebisho na marekebisho ya mwisho yalifanyika mwaka 2010 .
“Hata
kifungu cha 2 (3) cha sheria ya Judicuture and Application of Law
(JALA), inakataza matumuzi ya sheria za nje kutumika kuamua kesi za
uchaguzi wakati nchi yetu ina sheria mahususi ya uchaguzi kwa ajili ya
kuamua kesi za uchaguzi na kwamba jaji alikuwa sahihi kusema hilo na pia
alikuwa sahihi kusema wajibu rufaa walikuwa na haki ya kufungua kesi
hiyo na kuongeza kuwa hoja hiyo ni butu,” alidai wakili Mugwai.
Hata
hivyo, alipinga hoja ya mawakili wa Lema iliyodai Jaji Rwakibalila
katika hukumu yake hakutumia kesi walizoziwasilisha mbele yake, ambapo
alidai katika hukumu hiyo alitumia baadhi ya kesi walizoziwasilisha
mbele yake na kwamba jaji ana mamlaka ya kuchuja kesi anazotaka
kuzitumia kwenye hukumu.
Akijibu
hoja kwamba hukumu ya Lema iliegemea kwenye ushahidi wa mazingira tu,
wakili Mugwai alikanusha na kusema hakukuwepo ushahidi wa mazingira
kwani mashahidi waliomsikia Lema akitoa maneno ya kashfa kwenye mikutano
ya hadhara, walifika mahakamani hapo na kutoa ushahidi wao ambapo
walisema walimwona na kumsikia akfanya hivyo dhidi ya Batilda.
Hata
hivyo wakati wakili Mugwai akiwasilisha hoja zake, baadhi ya watu
wanaodaiwa ni wafuasi wa CHADEMA ambao walijazana ndani ya chumba cha
mahakama, waliguna na kutoa vicheko hali iliyosababisha wakili huyo
awaombe majaji wawadhibiti watu wenye tabia hiyo kwani mawakili wa Lema
walipokuwa wakiwasilisha hoja zao walitulia.
Rufaa
hiyo inayovuta hisia za wengi ndani na nje ya nchi, ilianza kusikilizwa
majira ya saa tatu asubuhi na kumalizika saa tisa alasiri.
Kesi hiyo imeahirishwa na sasa kinachosubiriwa ni tarehe ya hukumu ili kukata mzizi wa fitina.
Kwa
mujibu wa jopo hilo la majaji wa Mahakama ya Rufaa, tarehe ya kutolewa
uamuzi wa rufaa hiyo itatolewa kwa njia ya maandishi kwa mawakili wa
pande zote mbili.

No comments:
Post a Comment