MABINGWA
wa Tanzania Bara, Simba SC wameanza vyema michuano ya Kombe la
Mapinduzi, baada ya kuwachapa mabingwa wa Zanzibar, Jamhuri ya Pemba
mabao 4-2 usiku huu kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Hadi
mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana mabao 2-2, zikicheza
huku zikinyeshewa na mvua iliyoanza kabla hazijaingia uwanjani.
Jamhuri ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 17, mfungaji Mfanyeje Mussa Yussuf kwa shuti la umbali wa mita 17.
Simba
ilisawazisha bao hilo dakika ya 27, mfungaji Haruna Athumani Chanongo
aliyeunganisha kwa kichwa kona maridadi iliyochongwa na kiungo Kiggi
Makassy kutoka wingi ya kulia.
Baada
ya bao hilo, Simba walizidisha mashambulizi langoni mwa Jamhuri na
iliwachukua dakika mbili zaidi kupata bao la kuongoza, baada ya Chanongo
kufumua shuti kali akiwa umbali wa mita 20 upande wa kushoto mwa
Uwanja, ambalo lilimshinda mlinda mlango Jaffar Said.
Huku
ikielekea kama Simba itatoka uwanjani baada ya ngwe ya kwanza ikiwa
inaongoza 2-1, Mfanyeje tena aliwainua vitini wapenzi wa timu hiyo ya
Chasasa, Pemba kwa bao tamu la kusawazisha akimalizia mpira wa adhabu
uliopigwa na Abdallah Athumani, akamtungua kiulaini kipa wa Simba,
William Mweta.
Kipindi
cha pili, Simba walirudi kwa kasi ya kusaka bao la ushindi iliwachukua
dakika 12 tu kufanikisha malengo yao, baada ya Nahodha wa timu hiyo leo,
Shomary Kapombe aliyecheza kama kiungo mkabaji badala ya beki wa kati,
kufunga kwa shuti la chini la mpira wa adhabu.
Adhabu
hiyo ilifuatia mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu
Jr. kufanyiwa madhambi nje kidogo ya eneo la hatari na beki mmoja wa
Jamhuri.
Sunzu
aliwainua vitini wapenzi wa Simba dakika ya 66, baada ya kuuwahi mpira
uliokuwa unaelekea kutoka nje na kugeuka nao kuutumbukiza nyavuni
kiufundi.
Kabla
ya mchezo huo, Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad
alizindua mashindano hayo kwa kupiga penalti na kumfunga kipa wa
Jamhuri, Jaffar. Akiongozwa na raisi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA),
Aman Ibrahim Makungu, Mh Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF,
alizikagua timu zote mbili kabla ya kuanza kucheza.
Kocha
mpya wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig alikuwa jukwaani akiishuhudia
timu, ikiongozwa na watakaokuwa wasaidizi wake, Mganda Moses Basena na
mzalendo, Jamhuri Kihwelo.
Katika
mchezo wa leo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; William Mweta, Miraj Adam,
Paul Ngalema, Mussa Mudde/Abdallah Seseme dk81, Komabil Keita, Shomary
Kapombe, Haroun Chanongo, Mwinyi Kazimoto/Jonas Mkude 67, Felix
Sunzu/Ramadhan Singano dk81, Haruna Moshi na Kiggi Makassy/Christopher
Edward dk27.
Jamhuri
FC; Jaffar Said/Suleiman Maabad dk 75, Msafiri Leonard, Hamad Omar,
Hussein Omar, Mfaume Shaaban, Soud Amoud, Bakari Hamisi, Ally
Bilal/Mbara Ali dk82, Ally Ahmed ‘Shiboli’, Mfanyeje Mussa na Abdallah
Athumani.
Katika
mchezo uliotangulia, Tusker ya Kenya iliichapa Bandari ya hapa mabao
5-1, mabao ya Jesse Were 29 na 43, Ismail Dunga 35 Michael Olunga dakika
ya 89 na Andrew Tolowa dakika ya 90, wakati la Bandari lilifungwa na
Amour Janja dakika ya 83.
No comments:
Post a Comment