Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepokea silaha mbalimbali
yakiwamo mapanga, visu, majembe, sufuria, makoleo na sufuria kama
kilelezo katika kesi inayomkabili Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake
49. Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka manne likiwamo la wizi wa
mali yenye thamani ya Sh. milioni 59.6, uchochezi na kuingia kwa jinai
katika ardhi inayomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd kwa nia ya
kujimilika isivyo halali.
Vielelezo
hivyo vilitolewa na shahidi ambaye ni mpelelezi kutoka Mkoa wa Kipolisi
Temeke, jijini Dar es Salaam, Thobias Walelo (34), mbele ya Hakimu
Mkazi Victoria Nongwa.
Mbali na
silaha hizo, pia shahidi huyo aliwasilisha mahakamani hapo jenereta,
mabegi mawili ya nguo, nyundo na ndoo za plastiki ambavyo vilipokelewa
kama vielelezo vya kesi hiyo.
Alidai kuwa Oktoba 12, mwaka jana, majira ya alasiri, alipokea jalada kutoka kwa bosi wake kwa ajili ya kulifanyia kazi.
“Nilipolisoma
lilikuwa na taarifa kwamba kiwanja cha kampuni ya Agritanza Ltd
kimevamiwa na Sheikh Ponda na wenzake,” alidai shahidi.
Shahidi
huyo ambaye ni wa 10 wa upande wa mashitaka, alidai kuwa yeye alikuwa
mhusika kupeleleza jalada hilo, akishirikiana na D/Ssgt Juma na D/Koplo
Furaha, kwa kupitia maelezo ya mlalamikaji na nyaraka za mabadilishano
ya ardhi hiyo kati ya kampuni ya Agritanza Ltd na Bakwata.
Alidai
kuwa yeye mwenyewe alikwenda Manispaa ya Temeke kwa Bwana Ardhi
kufuatilia ukweli wa nyaraka hizo za mabadilishano ya ardhi na kupewa
majibu kuwa eneo hilo linamilikiwa kihalali na kampuni ya Agritanza
Ltd.
No comments:
Post a Comment