Fundi magari, David Kweka baada ya kupigwa risasi.
Tukio
hilo la aina yake, limetokea katika baa ya Dolphin, Sinza Kumekucha
jijini Dar baada ya shabiki mmoja wa Man United kuchomoa bastola na
kuzua kizaazaa hicho.
Kwa
mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, David alifika Sinza akiambatana na
kaka yake, Elnadia Kweka kwa ajili ya kuangalia mechi hiyo iliyokuwa
inaoneshwa katika runinga ya baa hiyo na wote walikuwa wakishabikia
klabu ya Chelsea.
Wakati
Man United ikiwa inaongoza mabao 2-0, mashabiki wa timu hiyo walikuwa
wakitamba na kutoa maneno ya kejeli kuonesha kwamba wao ndiyo wababe wa
soka nchini England.
David na kaka yake hawakuwa na la kusema hadi Chelsea iliposawazisha mabao hayo na ubao wa matokeo kusomeka 2-2.
Pamoja
na hali hiyo, mashabiki wa Man United waliendeleza tambo kwa kudai
kwamba lazima watapata bao la tatu wakati wowote na kumaliza mchezo huo
wakiwa washindi.
Jeraha katika mkono wa David Kweka.
Wakati
tambo hizo zikiendelea, Elnadia alishikwa na haja ndogo na kutaka
kwenda msalani, ndipo mtu aliyejulikana kwa jina moja la Wambura
aliyekuwa akishabikia Man United alipomzuia na kumwambia kuwa alikuwa
akitaka kukimbia.
“Ulitokea
ubishi mkubwa kati ya Elnadia na Wambura ambaye alijitambulisha kama
afisa usalama na ulipozidi, shabiki huyo wa Man United alichomoa bastola
na kumtishia.
“Hali
hiyo ilizua kizaazaa ndipo David alipoamua kumvaa Wambura na kutaka
kumnyang’anya bastola yake ili kumuokoa kaka yake. Wawili hao
walinyang’anyana bastola hiyo kwa muda mrefu hadi ilipofyatuka risasi
tatu kwa bahati mbaya,” alisema shuhuda mmoja.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, risasi moja kati ya hizo ilimpata David katika mkono wake wa kulia.
Watu
walitawanyika na baada ya muda David alichukuliwa na kupelekwa
Hospitali ya Palestina ambako alishonwa nyuzi 12 katika mkono wake.
Taarifa
zaidi za tukio hilo zinasema kuwa David alipoteza shilingi milioni moja
la laki saba ambazo alipewa na mteja wake kwa ajili ya kwenda
kumnunulia ‘gear box’.
Habari
zaidi zinasema, jalada la kesi hiyo limefunguliwa katika Kituo cha
Polisi cha Urafiki, Ubungo jijini Dar kwa namba URP/RB 17878/2013,
KUJERUHI KWA SILAHA.
Kwa
mujibu wa askari mmoja wa kituo hicho ambaye hakutaka kutajwa jina lake
gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa jeshi hilo, Wambura anashikiliwa
katika kituo hicho.
No comments:
Post a Comment