Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda leo Jumamosi, Machi 2, 2013 amezindua Tume maalum
aliyoiunda ili ifanye uchunguzi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne
yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu na kuwataka wajumbe wa Tume hiyo
watafute kiini cha mserereko wa kushuka kwa ufaulu kuanzia mwaka 2010
hadi 2012.
Waziri Mkuu amezungumza na wajumbe wa Tume
hiyo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni, jijini Dar es
Salaam. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa.
Amesema kwa mujibu wa hadidu za
rejea, wajumbe wa tume hiyo watatakiwa kuangalia ni sababu zipi
zimechangia kuwepo kwa matokeo hayo mabaya, mserereko wa kushuka umekuwa
ukiongezeka kwa sababu gani, usimamizi katika Halmashauri ukoje,
ukaguzi wa elimu na uhamishiwaji wa sekta ya elimu kwenye Wizara ya
TAMISEMi umechangiaje kushuka kwa kiwango cha ufaulu.
Vilevile, watatakiwa kuangalia
mitaala na mihutasari ikoje, kuangalia uwiano uliopo kwenye mitihani
inayotungwa ikiwa ni pamoja na uhakiki wa mitihani hiyo; kuangalia
mazingira ya kufundishia, mfumo wa upimaji, usimamizi na uendeshaji, na
kutokuwepo kwa chakula shuleni kunachangiaje kushuka kwa utendaji mbaya
wa wanafunzi katika masomo yao.
Tume hiyo yenye wajumbe 15, imepewa
muda wa wiki sita kuanzia Machi mosi iwe imekamilisha kazi hiyo na
kuwasilisha taarifa yao kwa Waziri Mkuu.
Tume itaongozwa na Prof. Sifuni
Mchome wa Tume ya Vyuo Vikuu, na Makamu wake atakuwa Bi. Bernadetha
Mushashu (Mbunge wa Viti Maalum – Kagera).
Wajumbe wengine ni Bw. James
Mbatia (mbunge wa Kuteuliwa), Bw. Abdul J. Marombwa (Mbunge wa Kibiti),
Prof. Mwajabu Possi (Chuo Kikuu - UDSM), Bibi Honoratha Chitanda (CWT),
Bibi Daina Matemu (TAHOSSA) na Bw. Mahmoud Mringo (TAMONGSCO).
No comments:
Post a Comment