Dar es
Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo amelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kile
alichosema kwamba limeshindwa kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani na
mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Kadhalika kiongozi huyo alihoji ulipofikia upepelezi wa mauaji ya
Padri Evarist Mushi wa Zanzibar aliyepigwa risasi mwezi uliopita huku
akisema, “Siwezi kusema naridhika au siridhiki lakini tulitegema kwamba
polisi wangetegua kitendawili cha wauaji wa padri huyo.”
Kardinali Pengo alisema Serikali haipaswi kusema wanaovuruga amani ni
wahuni wakati hilo ni jukumu lake kuhakikisha inadumisha amani. Pengo
alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam
wakati akitoa salamu za Pasaka.
“Watu wanaharibiwa mali zao, watu wanapoteza uhai wao, Serikali
haiwezi kukaa pembeni na kufikiri ni kauli za viongozi wa dini peke yao,
viongozi wa dini hawana jeshi au hawawezi kukamata watu, Serikali ndiyo
wana jukumu hilo kuhakikisha wanaingilia kati,” alisema Pengo na
kuongeza:
“Wengine wanasema si mapambano ya dini ya Kikristu na Waislamu ila ni
wahuni wachache wanajichukulia madaraka, lakini lolote liwavyo Serikali
haiwezi kukwepa majukumu yake, hatuwezi kutegemea nchi itawaliwe na
wahuni kama vile Serikali haipo.”
No comments:
Post a Comment