SIRI YA KUUWAWA
ZITTO
Katika gazeti la
Mtanzania toleo na. 7269 la Jumatano Machi 27, 2013 kuna habari yenye kichwa
chenye maneno ‘ SIRI YA KUUWAWA ZITTO YAFICHUKA’ na vichwa vidogo ‘yadaiwa
ilipangwa anyweshwe sumu hotelini’ dk. Slaa atajwa kumtuma Saanane kummaliza’.
Habari hii imeniletea usumbufu mkubwa kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga
kura wangu, wamejazwa na wasiwasi mkubwa sana kwamba ninaweza kuuwawa. Napenda
kusema yafuatayo:
Moja, sijawahi
katika maisha yangu yote kukutana na mtu anayeitwa Ben Saanane na hivyo hicho
kikao ambacho inasemekana nilikuwa naye na akajaribu kunipa sumu hakijawahi
kutokea. Imetajwa Hoteli ya Lunch Time ambayo sio tu sijawahi kufika, pia hata
siijui ipo wapi. Haijawahi kutokea mimi kufanya kikao cha pamoja na Ben
Saanane, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya
kufikirika na hivyo naomba mwandishi ahakikishe kuwa vyanzo vyake vya habari
vimempa habari sahihi.
Pili, Siamini kamwe
kuwa Katibu Mkuu wa chama changu anaweza kupanga kuniua maana hana sababu ya
kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba mimi ninaamini kuwa kila nafsi
itaonja mauti. Kila mtu atakufa. Kama nitakufa kwa kuuwawa na mtu mwingine ndio
itakuwa nimeandikiwa hivyo na Mungu. Ndio maana hata siku moja silalamiki
kuhusu vitisho vya kuuwawa nk. Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndio
furaha ya maisha yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili
lakini mawazo, fikra na maono ya Zitto yataishi tu. Siogopi kufa maana maisha
niliyoyachagua ndio haya ambayo yamejaa vitisho. Muhimu kwangu ni kufanya kazi
zangu kwa bidii, uhodari na uaminifu. Siku zote nitasimamia ukweli bila kujali
uchungu wa ukweli huo.
Tatu, nawashauri
watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine watumie muda wao kujenga
vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia masuala ya chama ambacho wao sio
wanachama tena. Kama mtu kaamua kuhama CHADEMA anapoteza haki ya kujadili
masuala ya CHADEMA maana kama angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya
mtu yeyote ambaye anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa.
CHADEMA sio pango la watesaji wala wauaji. Kama kuna mwanachama wa chama
kingine cha siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu
aende kwenye vyombo vya sheria kumshtaki. Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe
propaganda kama ni malengo ya taasisi.
Nne, Nawashauri viongozi wa CHADEMA na hasa
wanachama tutumie muda wetu kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu,
uongo, uzandiki nk kamwe havijengi chama. Chama chetu lazima kiwe mfano bora wa
kuheshimu demokrasia na haki za binaadamu. Wananchi hawawezi kutoa dola kwa
chama chenye mifarakano. Tusiruhusu kugawanywa kwa matakwa ya watu wachache. Tusimamie misingi
ya kuanzishwa chama chetu.
--
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar-es-Salaam
Jumatano, Machi 27, 2013
No comments:
Post a Comment