Mwanamume
anayedaiwa kuwa mfuasi sugu wa ODM alijinyonga katika kaunti ya Migori
akisema hawezi kuvumilia kuendelea kuishi bila kumwona Bw Raila Odinga
akiwa rais wa Kenya
MWANAUME alijinyonga katika kaunti ya Migori akisema hawezi kuvumilia kuendelea kuishi bila kumwona Bw Raila Odinga akiwa rais wa Kenya.
Mwanaume huyo alichukua hatua hiyo isiyo ya kawaida baada ya Mahakama ya Juu kuidhinisha ushindi wa Bw Uhuru Kenyatta kuwa rais wa Kenya.
Mkuu wa polisi eneo hilo Bw Richard Bitonga alisema mwanaume huyo alijitia kitanzi nje ya nyumba yake katika kituo cha kibiashara cha Lwanda, eneo bunge la Nyatike.
“Alianza kwa kuvalia jezi la chama cha ODM iliyokuwa na picha ya Waziri Mkuu kabla ya kujitia kitanzi,” akasema Bw Bitonga. Ingawa mwanaume huyo hakuacha ujumbe wowote, alikuwa amewaeleza marafiki wake kwamba alikasirishwa na uamuzi wa mahakama.
Bw Bitonga alisema mwanaume huyo aliye na mke amekuwa mfuasi sugu wa ODM eneo hilo.
Baadhi ya wakazi walisema marehemu alikuwa ametisha kujitoa uhai ikiwa Bw Odinga hangeshinda kesi ya kupinga uchaguzi wa urais. “ Alisema hakuona sababu ya kuendelea kuishi katika ulimwengu huu ikiwa Bw Odinga hatakuwa rais wa nchi hii,” alisema mkazi Bw Samuel Otieno, aliye mchimba dhahabu.
No comments:
Post a Comment