Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba.
CHAMA cha Wananchi (CUF) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) wameingia katika mvutano mkali kuhusu mateso yanayodaiwa
kufanywa na askari wa jeshi hilo dhidi ya viongozi wa chama hicho na
raia mkoani Mtwara.
Wakati CUF wakizitaka asasi za kiraia zinazoshughulikia haki za
binadamu na haki za wanawake kumsaidia kisaikolojia mwanamke anayedaiwa
kubakwa na askari wa JWTZ mkoani humo, jeshi hilo limeonya kuwa tukio
hilo ni la kupandikizwa.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, JWTZ imewataka wananchi
wapuuze taarifa hizo zinazofanywa na watu wenye malengo ya kulichafua
jeshi.
Wakati JWTZ ikitoa taarifa hiyo, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba, amesema askari wa jeshi hilo waliopo Mtwara wamekuwa wakifanya
vitendo vya kihalifu ikiwemo kutesa, kubaka na kuwapiga watu.
Lipumba alisema kutekwa kwa Naibu Mkurugenzi wa CUF Taifa, Shaweji
Mketo na viongozi wengine wa chama hicho Mkoa wa Mtwara, ni kinyume cha
sheria na kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho
jijini Dar es Salaam jana, Lipumba alisema wanafanya mchakato wa
kushughulikia uonevu huo wa JWTZ.
Profesa Lipumba alisema mbali ya Mketo, viongozi wengine waliotekwa
na kuteswa ni Salum Hamis Mohamed (Mwenyekiti CUF Mtwara Mjini),
Ismail Hamis Jamal (Mwenyekiti CUF Mtwara Vijijini), Ismail Bakari
Njalu (Mwenyekiti wa Vijana -JUVICUF Mtwara Mjini), Said Issa Kulaga
(Katibu CUF Mtwara Mjini) na Kashindye Kalungwana (Dereva wa CUF Ofisi
Kuu)
Alisema katika hatua hizo, watahakikisha waliohusika na unyama
dhidi ya mwanamke huyo wanafikishwa mahakamani ili sheria ichukue
mkondo wake.
Alieleza kuwa, viongozi hao baada ya kutekwa na askari wa JWTZ,
walivuliwa nguo zote na kulazwa kifudifudi, kumwagiwa maji ya baridi na
kupakwa chumvi kisha kuanza kupigwa usiku kucha kwa kutumia mikanda ya
jeshi, ngumi, mateke, fimbo maalumu za ngozi za wanyama na miti
maalumu.
Akielezea tukio hilo, Profesa Lipumba alisema viongozi hao wakiwa
njiani kurejea Mtwara mjini wakitokea Msimbati, ghafla waliona magari
mawili ya kijeshi ambayo baada ya kuona gari la CUF lenye namba T 886
BGW, waliziba barabara na askari wa JWTZ waliwashusha na kuanza
kuwapiga na kisha kuwarusha kwenye karandinga la jeshi.
Alisema baadaye viongozi hao walipelekwa katika kambi ya jeshi ya
Naliendele kabla ya kuachiwa majira ya saa 5:00 usiku kwa kukabidhiwa
kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara ambaye hadi anakabidhiwa viongozi
hao, alikataa kutoa ushirikiano kwa CUF.
Alisema Mketo alipozinduka Juni 28 alijikuta ana dripu na hakuelewa ni ya nini na baadaye wanajeshi waliitoa.
Profesa Lipumba alisema tukio la utesaji raia ndani ya kambi ya jeshi
ukiliunganisha na matukio mengine kama ya uteasaji wa Dk. Stephen
Ulimboka, kutekwa nyara kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF),
Absalom Kibanda, kulipuliwa bomu katika mkutano wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) kunadhihirisha hatua za awali za kusambaratika
kwa dola.
Licha ya malalamiko hayo, taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya
Habari na Uhusiano ya Jeshi la Wananchi, ilieleza endapo taarifa hizo
zitatangazwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari wananchi wazipuuze,
kwani hazina ukweli wowote zaidi ya kuwa ni za upotoshaji.
Kauli ya jeshi ilisema: “Msichana huyo amepandikizwa ili kuharibu
taswira nzuri ya JWTZ. Ifahamike kwamba maofisa na askari wa JWTZ
waliopo Mtwara wanafanya kazi kwa uangalizi wa karibu, na vitendo hivyo
vya aibu hawawezi kuvifanya. Jeshi letu linafanya kazi kwa nidhamu na
si kama baadhi ya watu wenye maslahi binafsi wanavyolipaka matope.”
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment