Kiongozi wa Uamsho, Shekhe Faridi Ahmed. |
Mawakili
wa Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu ya Zanzibar
(Jumiki), Shekhe Faridi Ahmed (41) na wenzake tisa wameiomba Mahakama
kufuta taarifa ya kukata rufaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka wa Zanzibar
(DPP).
Waliomba hayo
jana katika Mahakama ya Rufaa Dar es Salaam mbele ya Jopo la majaji
Januari Msoffe, Salum Massati na William Mandia, wakati wakisikiliza
ombi la kutaka rufaa dhidi ya uamuzi wa dhamana uliotolewa Machi 11
mwaka huu katika Mahakama Kuu ya Zanzibar litupwe.
Katika uamuzi huo, Mahakama ilitengua mwenendo wa maombi ya dhamana
ya washitakiwa pia ilitupilia mbali maombi ya marejeo ya uamuzi wa
Msajili wa Mahakama Kuu uliowanyima dhamana washitakiwa, pamoja na
kukataa pingamizi la awali la upande wa mashitaka.
Ombi hilo lilisikilizwa jana bila washitakiwa kufika mahakamani, huku
ulinzi ukiwa umeimarishwa katika eneo la Mahakama, ambapo kila mtu
aliyeingia alikaguliwa na mashine ya ukaguzi.
Wakili wa waleta maombi, Salum Toufiq alidai wameleta ombi hilo kwa
kuwa dhamana ni haki kwa washitakiwa na kwa mujibu wa Katibu ya
Zanzibar, kesi za jinai zinatakiwa kusilikizwa na kutolewa uamuzi
haraka lakini wanachofanya upande wa mashitaka ni kuchelewesha kesi.
Hata hivyo, mawakili wanaomwakilisha DPP walidai Msajili wa Mahakama
Kuu ya Zanzibar, aliyesikiliza maombi ya kwanza ya dhamana ya
washitakiwa hao, hakuwa na mamlaka kisheria ya kufanya hivyo.
Aidha, walidai maombi ya akina Farid si sahihi, kwa kuwa wameyaleta
kwa kutumia kifungu cha Kanuni za Mahakama ya Rufaa ambacho kinatumika
na Mahakama yenyewe.
Jaji Msoffe alipotaka maelezo kama Msajili aliyesikiliza maombi ya
kwanza ya akina Farid alipewa mamlaka na Jaji Mkuu ya kufanya hivyo,
mawakili wa waleta maombi walidai hakuwa nayo.
Wakili Ramadhan Nassib alidai uamuzi uliotolewa na msajili ulikuwa
batili na msajili huyo alichukua kesi bila ya kufuata utaratibu hivyo
haikuwa sahihi na kwamba kilichobaki Mahakama Kuu ni hati ya mashitaka
dhidi ya washitakiwa tu.
Mbali ya Shekhe Farid, waleta maombi wengine ni Mselem Ali Mselem,
Mussa Juma Mussa, Azan Khalid, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali
Suleiman, Hassan Bakar Suleiman, Ghalib Ahmada Jum,Abdallah Said na
Fikirini Fikirini.
Shekhe Farid na wenzake walifikishwa mahakamani Oktoba 25 mwaka jana
na kusomewa mashitaka chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa na Sheria ya
Kanuni za Adhabu na hawakuruhusiwa kujibu mashitaka yao.
Aidha walinyimwa dhamana kwa kuwa DPP aliwasilisha hati ya kuzuia
dhamana yao kwa madai kuwa watahatarisha usalama wa nchi. Washitakiwa
hawakuridhika na uamuzi huo na kuwasilisha maombi ya marejeo ya uamuzi
huo, lakini upande wa mashitaka uliweka pingamizi ukiomba maombi hayo
yatupiliwe mbali.
Jaji Abrahamu Mwampashi alitupilia mbali pingamizi hilo la upande wa
mashitaka, maombi ya marejeo ya washitakiwa na kubatilisha mwenendo wa
maombi ya dhamana kwa Msajili wa Mahakama Kuu.
No comments:
Post a Comment