Jeshi la
Polisi mkoani Mtwara limemkamata mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain
Murji likimtuhumu kuchochea vurugu za kupinga mradi wa bomba la gesi
kutoka mkoani humo kwenda jijini Dar es Salaam.
Habari
zilizopatikana na kuthibitishwa na Msemaji wa Jeshi la polisi nchini,
Advera Senso zinaeleza kuwa Murji alikamatwa jana jioni nyumbani kwake
maeneo ya Shangani mjini Mtwara.
Kukamatwa kwa
mbunge huyo kunakuja ikiwa zimepita siku tano tangu viongozi wanne wa
vyama vya upinzani mkoani Mtwara, kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mtwara, Juni 4, mwaka huu wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwamo kula
njama, kufanya uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wakazi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Washtakiwa
hao ni Katani Ahmed Katani (33) na Saidi Kulaga (45) wa CUF, Hassan
Uledi (35) wa NCCR Mageuzi na Hamza Licheta (51) wa TLP, wote wakazi wa
Mtwara.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa baada ya polisi kumkamata mbunge huyo,
walifanya upekuzi katika nyumba yake kwa saa kadhaa na baada ya
kujiridhisha walikwenda kupekua na ofisi yake.
“Amekamatwa
kwenye saa 11:00 jioni, hata hati ya kukamatwa kwake imeeleza kuwa
anatuhumiwa kuchochea vurugu za kupinga gesi inayopatikana mkoani Mtwara
kwenda Dar es Salaam,” alisema Katibu wa Mbunge huyo, Meckland Millanzi.
Katika ufafanuzi wake Senso alisema kukamatwa kwa mbunge huyo ni
jambo la kawaida na kwamba hivi sasa unaandaliwa utaratibu ili faili
lake lipelekwe kwa Mwanasheria wa Serikali.
“Acheni
polisi ifanye kazi yake kama kutakuwa na la ziada tutawaeleza ila kwa
sasa tunaandaa utaratibu wa suala hili kwenda kwa mwanasheria wa
Serikali,” alisema Senso.
Murji amekamatwa ikiwa zimepita siku 16 tangu kutokea vurugu kubwa
mkoani Mtwara zilizodumu kwa siku mbili, ambapo polisi walipambana na
makundi ya vijana wanaopinga mradi wa bomba la gesi kujengwa.
Vurugu hizo zilizosababisha baadhi ya watu kupoteza maisha huku
wengine wakiachwa majeruhi na mali nyingi kuharibiwa, ziliibuka baada ya
hotuba ya bajeti ya wizara ya nishati na madini kusomwa bungeni .
Mvutano kuhusu mradi wa bomba la gesi ulianza Novemba 16, mwaka jana
baada ya Serikali kutuma kamati inayoratibu maoni ya sera ya gesi “The
Natural Gas Policy of Tanzania -2013” ambayo ilifika mkoani Mtwara
kukusanya maoni ya wananchi.
Katika mikutano yake mjini Mtwara, wananchi wengi hawakukubaliana na
wazo la kusafirishwa gesi nje ya Mtwara kwa njia ya bomba. Hali hiyo
ndiyo iliyowasukuma viongozi wa vyama kuhamasisha wananchi kuhusu suala
hilo
No comments:
Post a Comment