Mtuhumiwa wa Kesi ya Kuiba na Kughushi Benki akiondoka Mahakamani
**********************
MTU mmoja aliyefahamika kwa
jina la Deogratius Mpembe amehukumiwa kutumikia kifungo cha Miaka 20 Jela kwa
kosa la kughushi nyaraka za kutolea fedha katika Benki ya CRDB Tawi la
Mwanjelwa Jijini Mbeya.
Hukumu hiyo imetolewa jana na
Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya Gilbert Ndeuruo, baada ya kumtia hatiani
Mshtakiwa kwa makosa 14 ambayo Mtuhumiwa
alikubali kutenda baadhi ya makosa na mengine kuyakanusha.
Mwendesha mashtaka wa Serikali
Lugano Mwakilasa aliiambia mahakama hiyo kuwa Mshtakiwa alitenda makosa hayo katika
vipindi tofauti kati ya Mwezi Juni, 2011 kinyume cha kifungu cha 235 Sura ya 20
ya Mwaka 2002 ya kanuni ya adhabu.
Mwakilasa alisema Mtuhumiwa
alipatikana na Kosa la kughushi nyaraka za kutolea fedha katika Benki ya CRDB
katika akaunti mbili za mteja wa benki hiyo ambaye ni marehemu Clemence Kihanga
ambaye imedaiwa mahakamani hapo kuwa na uhusiano na Mshtakiwa.
Mbali na kosa hilo Mtuhumiwa
huyo pia anadaiwa kuiibia Benki hiyo
fedha za kigeni Dolla za Marekani 118,137.4 pamoja na fedha za kitanzania
Shilingi Milion 2,468,181.24 ambapo
Mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo akiwa ni karani wa Benki hiyo akiwa na
kitambulisho cha kazi chenye namba CK
4M.
Upande wa Mashtaka ulikuwa na
mashahidi wanne ambao ni Meneja wa benki hiyo tawi la Mwanjelwa Ephraim Luwila,
Mtaalamu wa maandishi kutoka Jeshi la Polisi namba E2912 Johanes, Mke wa
Marehemu Niku Kihanga na Kaimu Meneja wa Benki hiyo Alfred Basajile.
Katika maelezo yao Mashahidi
hao walitoa Vielelezo mbali mbali mahakamani hapo kama sehemu ya ushahidi
ikiwemo Kitambulisho cha kazi cha Mtuhumiwa, Hati ya Kifo cha marehemu
aliyefariki Novemba 2010 na Nyaraka za maandishi ambazo zote zilikuwa na
miandiko inayofanana na Mtuhumiwa kama vile Mkato na Sahihi zake.
Awali ilielezwa kuwa
kugundulika kwa wizi wa fedha hizo ni baada ya Mke wa Marehemu Niku Kihanga
kufuatilia masalio ya akiba ya Mume wake baada ya kuidhinishwa kuwa msimamizi
wa mirathi na kuomba kupewa masalio ya akiba zote na kukuta kuna upungufu wa Dola
5000 kwa akaunti ya fedha za nje na akaunti ya ndani ikikutwa na Shilingi 36,000/=
badala ya Shilingi 2,400,000/=.
Mke wa marehemu alisema
kufuatia kuwepo kwa upungufu mkubwa wa fedha hizo aliamua kupeleka malalamiko
kwa Meneja wa benki hiyo ambaye alianza kulifanyia kazi kwa kupeleka malalamiko
Polisi.
Kutokana na Ushahidi huo pamoja
na maelezo ya kukiri Polisi, Hakimu Gilbert Ndeuruo alimtia hatiani
Mtuhumiwa kwa makosa yote 14 na kumhukumu kila kosa kwa miaka Mitano ambapo
alisema Mtuhumiwa atatumikia makosa yote kwa pamoja kwa kwenda Jela Miaka 20.
Aidha kabla ya kutoa hukumu
hiyo Mwendesha mashtaka Lugano Mwakilasa aliiomba Mahakama hiyo kutoa adhabu
kali ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wasiokuwa waaminifu.
Hata hivyo Hakimu huyo kabla ya
kutoa hukumu alimtaka Mtuhumiwa huyo kujitetea ili apunguziwe adhabu ya kifungo
cha maisha kutokana na makosa aliyokutwa nayo, ambapo Mtuhumiwa huyo aliiomba
mahakama kumpunguzia adhabu kwa kile alichodai anasumbuliwa na ugonjwa wa
Kansa, Mtoto mmoja, Mkewe na Mdogo wake ambaye anamsomesha kuwa wanategemea
msaada wake.
Pamoja na utetezi huo ambao
Hakimu aliridhika nao na kumpunguzia adhabu kutoka Kifungo cha Maisha hadi
kumfunga kutumikia Jela kwa Miaka 20 na kuongeza kuwa anaruhusiwa kukata rufaa
endapo hatakuwa ameridhika na adhabu aliyopewa ndani ya Siku 30.
PICHA , HABARI NA MBEYA YETU BLOG
No comments:
Post a Comment