Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Dar es Salaam.
Serikali
imetangaza viwango vipya vya chini vya mishahara kisekta ambavyo
vinatofautiana kati ya sekta moja na nyingine ambavyo ni kuanzia
Sh40,000 hadi Sh400,000 kwa mwezi kuanzia Julai Mosi mwaka huu.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Kazi na Ajira,
Ridhiwani Wema, watakaolipwa kima kidogo zaidi cha Sh40,000 ni
wafanyakazi wa nyumbani ambao wameajiriwa na watu wa kawaida huku
wakiishi kwenye nyumba za waajiri wao.
Kwa
upande mwingine, katika viwango hivyo, kima kikubwa katika viwango hivyo
cha Sh400,000 kitalipwa kwa wafanyakazi wa sekta za mawasiliano
zikiwamo kampuni za simu, kampuni za kimataifa za nishati, madini na
taasisi za fedha.
Katika
viwango hivyo, mishahara kwa wafanyakazi wa nyumbani walioajiriwa na
watu wa kawaida lakini ambao hawaishi kwenye nyumba za waajiri wao
itakuwa Sh80,000.
“Viwango
vya chini vya mishahara kwa wafanyakazi wa nyumbani walioajiriwa na
mabalozi wa kigeni na wafanyabiashara maarufu wanatakiwa kulipwa
Sh150,000 kwa mwezi,” ilisema taarifa hiyo.
Wafanyakazi wa nyumbani walioajiriwa na maofisa wa Serikali watalipwa Sh130,000 kwa mwezi.
Kima cha chini cha mshahara katika huduma za kilimo ni Sh100,000 na huduma za afya Sh132,000.
Kwa
upande wa wafanyakazi wa vyombo vya habari, posta na usafirishaji wa
vifurushi ‘courier services’, kima cha chini kitaanzia Sh150,000.
Viwango
vya chini vya mishahara kwa wafanyakazi wa hoteli za kitalii kuanzia
Julai Mosi, mwaka huu ni Sh250,000, wakati kwa hoteli za kati ni
Sh150,000 na migahawa, nyumba za wageni na baa ni Sh130,000.
Kampuni
za ulinzi za kimataifa zitapaswa kulipa kiwango cha chini cha mishahara
cha Sh150,000 kwa wafanyakazi wake sawa na kampuni ndogo za huduma za
nishati. Kampuni ndogo za ulinzi zitatakiwa kulipa Sh100,000.
Kima
cha chini kwa wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa anga kitakuwa
Sh300,000, sawa na wale wa utoaji na uingizaji wa mizigo. Wafanyakazi
wanaofanya katika sekta ya usafirishaji wa majini, uvuvi na nchikavu
wakitakiwa kulipwa Sh200,000.
Kima
cha chini kwa kampuni za makandarasi daraja la kwanza kitakuwa
Sh325,000, makandarasi daraja la pili hadi la nne Sh280,000 na
makandarasi daraja la tano hadi saba Sh250,000.
HABARI HII IMEHAMISHIKA KUTOKA GAZETI LA MWANACHI LEO
No comments:
Post a Comment