Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba akisaini hati na Mwenyekiti
wa Kampuni ya Uwekezaji ya CPI, Lu Quizhou baada ya kuingia mkataba wa
uwekezaji wa nishati ya Umeme jijini Dar es Salaam leo.
Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba akibadilishana hati na Mwenyekiti wa Kampuni ya Uwekezaji ya CPI, Lu Quizhou baada ya kuingia mkataba wa uwekezaji wa nishati ya Umeme kutoka China.
--
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
ameendelea kusisitiza na kuwataka wakazi wa mkoa wa Mtwara kuelewa kuwa Gesi
iliyopatikana katika mkoa huo ni kwa ajili ya Watanzania wote.
Akizungumza wakati akiwekeana makubaliano na kampuni ya
uwekezaji wa nishati ya umeme kutoka China (CPI), Profesa Muhongo alisema
kuwa hata kama wakazi wa mkoa huo watashindwa kuridhia uwekezaji wa nishati
hiyo lakini gesi hiyo ni kwa maendeleo ya Watanzania wote.
Profesa Muhongo alisema kuwa makundi yanayopinga matumizi
ya gesi hiyo yanapaswa kuweka hadharani mikakati yao kuliko wanavyofanya sasa
kwa kupinga pasipo kutoa mipango yao.
Alisema inapaswa kufika mahali Watanzania wakagawanywa
katika makundi mawili ikiwemo lile linalotaka maendeleo na linalopinga ili
waweze kutengewa maeneo.
“Hatuwezi kuondoa umaskini kama tusipotumia gesi na
raslimali tulizo nazo na hata hili tatizo linalolalamikiwa sasa la vijana
kukosa ajira litapata ufumbuzi kama tutaweza kupanua uchumi wetu,” alisema.
Alisema kuwa Watanzania wanapaswa waache kulazimisha
kufuata mawazo ya kupotosha.
“Tunataka uchumi ukue, tuwe na umeme wa uhakika na hata
bajeti yetu kuondoka katika kuongeza bei katika bidhaa ndogo ndogo ili linaweza
kufanikiwa kama tukiwa na umeme wa uhakika na kutumia gesi yetu,” alisema.
Aidha katika makubaliano hayo, Serikali imeingia
makubaliano na kampuni hiyo kwa kuzalisha umeme wa megawati 600 katika eneo la
Kinyerezi namba 3 lililopo jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa umeme huo utatumika kwa ajili ya matumizi ya
kawaida na ifikapo mwaka 2014 mwishoni wataweza kuuza megawati 500 kwa nchi za
nje zenye uhitaji wa nishati hiyo.
“Kupitia uzalishaji huo tunategemea mwaka 2016 tutaweza
kuzalisha megawati 1500 za nyongeza
hatua hiyo itaweza kubadilisha uchumi wetu na kuwa na bajeti yenye
uhakika zaidi,” alisema.
Profesa Muhongo alisema kuwa makubaliano hayo ambayo yanafanyika na Shirika la Umeme Nchi (Tanesco) na kampuni hiyo ya CPI utaweza kugharimu kiasi cha Dola milioni 300 hadi kukamilika.
No comments:
Post a Comment