Mkuu
wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini,Ofisi ya Rais Sekretariati ya
Ajira katika Utumishi wa Umma Bi. Riziki Abraham (kushoto) akizungumza
na vyombo vya habari nchini juu ya Uendeshaji wa Mchakato wa Ajira
katika Utumishi wa Umma, kwenye mkutano uliofanyika
leo katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO)Jijini Dar es Salaam,kulia
ni Katibu Msaidizi Idara ya Ajira kutoka Ofisi hiyo Bw. Malimi Muya.
Katibu
Msaidizi Idara ya Ajira kutoka Ofisi ya Rais Sekretariati ya Ajira
katika Utumishi wa Umma Bw. Malimi Muya (kulia) akifafanua jambo kwa
waandishi wa habari juu ya Uendeshaji wa Mchakato wa Ajira katika
Utumishi wa Umma, kwenye mkutano uliofanyika leo ukumbi wa Idara ya
Habari(MAELEZO) Jijini Dar es Salaam, katikati ni Mkuu wa Kitengo Cha
Mawasiliano Serikalini wa Ofisi hiyo Bi. Riziki Abraham na kushoto ni
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa.
…………..
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Anwani ya simu: “SEKRETARIET”, Ofisi ya Rais
E-mail; katibu@ajira.go.tz Sekretarieti ya Ajira
gcu@ajira.go.tz S.L.P. 63100
Tovuti: www.ajira.go.tz Dar es Salaam-Tanzania
Fax Na.: 2153518 16 Julai, 2013
Taarifa kwa Vyombo Vya Habari
Uendeshaji wa mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma
Sekretarieti
ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa
Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na
Sheria Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu 29 (1). Jukumu la msingi la
Sekretarieti ya Ajira ni kuendesha mchakato wa ajira katika Utumishi wa
Umma. Hapa ina maana kuwa jukumu la kuajiri, kuthibitisha watumishi
kazini pamoja na masuala ya nidhamu ya Watumishi yanabaki kwa Watendaji
Wakuu wa Wizara na Taasisi katika Utumishi wa Umma mitarafu ya Kifungu
cha 6(1) (b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma no 8 ya mwaka 2002. Ambapo
katika kuendesha mchakato huo, Sekretarieti ya Ajira inapaswa kuzingatia
Sheria, Kanuni, na Taratibu zilizopo ili kuhakikisha Utumishi wa Umma
unapata Watumishi weledi na wenye maadili mema. Hadi sasa jumla ya
waombaji 4891 tumeshaendesha mchakato wao wa ajira na kuwapangia vituo
vya kazi.
Hata
hivyo, Sekretarieti ya Ajira kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma ilipeleka Mswada Bungeni unaopendekeza
kukasimu madaraka ya kuendesha mchakato wa Ajira ili baadhi ya Waajiri
wakasimiwe madaraka hayo ili kurahisisha utendaji kazi katika
kushughulikia mchakato wa ajira kwa baadhi ya kada. Huku Sekretarieti
ya Ajira ikiendelea kuhakikisha kuwa jukumu hilo linaendelea kutekelezwa
kwa ufanisi. Tunapoongelea suala la ufanisi hapa Kitengo cha Udhibiti
na Ubora kinasimamia suala zima la uhakiki wa taarifa za mhusika,
uhakiki wav yeti na uadilifu wake kwa ujumla. Ambapo hadi sasa
tumeshakamata jumla ya vyeti vya kughushi 677 ambavyo wahusika wanadai
wamevipata kutoka RITA, VETA na NECTA.
Nafasi
wazi za kazi zitakazokuwa zikitangazwa na mchakato wake kuweza
kukasimiwa ni pamoja na Kada ya Wasaidizi wa ofisi, Wahudumu wa afya,
Madereva, Maafisa Watendaji wa Kata, Mtaa, Kijiji, Wapishi, Walinzi,
Madobi, Wasaidizi watunza kumbukumbu pamoja na Makatibu Muhtasi (walio
chini ya cheo cha mwandishi mwendesha ofisi) au Kada zingine ambazo
Katibu wa Sekretarieti ataona inafaa kukasimu.
Aidha,
nitoe ushauri kwa wanafunzi walioko shuleni na wanaotarajia kuingia
vyuoni kuchukua masomo ama kozi za fani ya Afya, Elimu, Mifugo na Kilimo
maana ni maeneo ambayo bado yana fursa nyingi za ajira Serikalini na
wahitimu wake pindi wamalizapo wanapangiwa vituo vya kazi moja kwa moja
bila ya kupitia mchakato wetu wa ajira kutokana na uhaba wa Wataalam wa
fani hizo katika soko la ajira hivi sasa.
Sekretarieti
ya Ajira katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kwa haraka zaidi
zinazohusu mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma na ili kuweza
kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya habari na
mawasiliano nchini na duniani kwa ujumla, iliamua kuanzisha tovuti yake (www.ajira.go.tz)
ambayo imerahisisha kwa kiasi kikubwa utoaji na upokeaji wa taarifa
mbalimbali hususani za matangazo ya fursa za ajira taarifa nyingine
zinazohusu masuala ya ajira Serikalini na matangazo mengine yanayohusu
shughuli za Sekretarieti ya Ajira. Tangu kuzinduliwa mwezi Aprili, 2013
imeweza kutembelewa na wadau zaidi ya 2,900,000.
Pamoja
na tovuti Sekretarieti ya Ajira imeanzisha KANZIDATA (DATABASE) za
aina tatu (3) ambazo ni Kanzidata ya Wahitimu wa Vyuo, Kanzidata ya
waliofaulu usaili na Kanzidata ya waliopangiwa vituo vya kazi.
Jambo
lingine ambalo ningependa mkalifahamu ni kuwa, Sekretarieti ya Ajira
iko katika hatua za awali za mchakato wa kuwawezesha waombaji wa fursa
za ajira kuwasilisha maombi ya kazi kwa mfumo wa kielektroniki
(e-application) kwa nafasi wazi zitakazokuwa zikitangazwa katika
Utumishi wa Umma ili kurahisisha kupunguza mlolongo wa uendeshaji
mchakato wa ajira ulivyo hivi sasa.
Mwisho
nimalizie kwa kuwataka waombaji wa fursa za ajira kutokuchagua maeneo
ya kufanyia kazi, hususani wale wanaopangiwa vituo vya kazi na
Sekretarieti ya ajira na hawaendi kuripoti bila ya kutoa sababu za
msingi maana Sekretarieti ya Ajira inaona hili ni kosa na inaandaa
utaratibu wa kutowaruhusu kufanya usaili mwingine waombaji kama hao.
Imetolewa
na Riziki V. Abraham, Msemaji na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
+255-687624975
No comments:
Post a Comment