MJUMBE wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Eddie Riyami, amesikitishwa na hatua ya kuvuliwa uanachama kwa aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mansour Yussuf Himid. Hata hivyo, mjumbe huyo amemshutumu Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, akisema kuwa ni mmoja kati ya wajumbe wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kutoka Zanzibar walioshiriki kikao hicho cha kumvua uanachama.
Akihojiwa na Radio ya Sauti ya Ujerumani (Deutsche Welle), katika kipindi Maalumu cha 'Meza ya Duara', Riyami alimtuhumu vikali Dk. Shein, akidai amekosa shukurani kwa Mansour na kumtaka kumuomba radhi. (HM)
"Shein amesahau kama Mansour ni mmoja kati ya Wazanzibari waliokwenda Dodoma kuhakikisha Dk. Shein anapita kuwania kiti cha urais wa Zanzibar, ili aendeleze maridhiano, namshangaa leo hii, Dk. Shein kuwa wa kwanza kupigania Mansour afukuzwe," alisema Riyami.
Katika mahojiano hayo, Riyami alimsifu Mansour kuwa ni miongoni mwa vijana shupavu ndani ya CCM waliohakikisha Zanzibar inaingia katika siasa za maridhiano na chama cha upinzani cha CUF na hivyo kuondokana na siasa za chuki na uhasama zilizodumu kwa muda mrefu visiwani humo.
Riyami alisema Mansour hakustahili kufanyiwa aliyofanyiwa, na kusisitiza maoni aliyokuwa akiyatoa akiitaka Zanzibar kuwa na dola yake kamili, yalikuwa ni maoni yake akiwa kama Mzanzibari.
Kauli hiyo ya Riyami imekuja siku chache baada ya Mansour kufukuzwa uanachama wa CCM na kikao cha NEC, kilichokaa wiki hii mjini Dodoma, akituhumiwa kutamka hadharani misimamo yake inayokinzana na CCM.
Mansour alituhumiwa na kikao hicho kwa kushindwa kusimamia malengo, madhumuni na masharti ya chama pamoja na kukiuka maadili ya kiongozi kwa kukiuka Ilani ya chama hicho ya mwaka 2010.
Hata hivyo, kabla ya hukumu ya Mansour mjini Dodoma, kulikuwa na hali ya mvutano wa chini uliokuwa ukiendelea kati ya Dk. Shein na wajumbe wa Kamati ya Maridhiano, inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Mzee Hassan Nassor Moyo.
Dk Shein aliwatuhumu wajumbe wa kamati hiyo kutoka CCM, akidai inakwenda kinyume na msimamo wa CCM unaotaka serikali mbili.
Dk. Shein anawatuhumu wajumbe wa kamati hiyo kutoka CCM ambao ni Mzee Moyo, Mansour na Riyami, pamoja na Aboubakar Khamis, Ismail Jussa na Salim Bimani, kwamba inawapotosha Wazanzibari juu ya muundo wa Muungano.
Katika moja ya mikutano yake ya kisiasa, Dk. Shein aliikana kamati hiyo na kusema haitambui na kuwataka wajumbe wake kuacha mara moja kile alichodai kutumia 'mgongo' wake katika kufikia malengo yao.
Katika mahojiano na Sauti ya Ujerumani, Riyami alisema kilichofanyika mjini Dodoma ni juhudi zinazoendelezwa na Dk. Shein za kutaka kuwaumiza wajumbe wa Kamati ya Maridhiano.
Riyami aliwatuhumu wajumbe wa NEC kutoka Zanzibar akisema, wamepatwa na 'kihoro' cha maridhiano yaliyofikiwa kati ya CCM na CUF, baada ya kuundwa kamati nyingi za muafaka ambazo hazikuzaa matunda.
"Hawa ndio wale wahafidhina waliokaa Dodoma kumfukuza Mansour, wamepatwa na kihoro, ziliundwa kamati za muafaka nyingi hazikuzaa matunda, kinachofanyika ni kisingizo cha kuwaumiza wajumbe wa kamati ya maridhiano," alisema Riyami.
Riyami alisema kitendo alichofanyiwa Mansour hakiwashangazi, akidai vikao vinavyofanyika mjini Dodoma ni sehemu ya 'machinjio' ya kuwamaliza Wazanzibari.
Alitaja baadhi ya vikao vya NEC vilivyowahi kufanyika mjini Dodoma na kuamuru kuwafukuza unachama wa CCM, Maalim Seif Sharrif Hamad, Marehemu Shaban Mloo, Haji Duni, Marehemu Soud Yusuf Mgeni na aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi Zanzibar, Ramadhan Fakih.
Riyami alikumbusha tukio la mwaka 1984, ambako kulifanyika vikao vya NEC na kuamuru kumvua nyadhifa zake zote za urais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, akidaiwa kutaka kuusaliti Muungano.
"Haya ya Mansour wala hatuyashangazi...wala si ya ajabu na hili nalisema wazi pasipo na shaka, sitanii, Shein amwite Mansour amuombe radhi hadharani kwa kumdhalilisha mwanasiasa shupavu.
Leo wajumbe wa Kamati ya Maridhiano wanakutana katika Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar, kuzungumzia hatima ya kufukuzwa mjumbe mwenzao, Mansour, huku katika kikao hicho kitakachohudhuriwa na wajumbe wa CUF, Mansour anatarajiwa kutoa yaliyo moyoni mwake juu ya kadhia ya kufukuzwa kwake uanachama wa CCM. Chanzo: mtanzania
No comments:
Post a Comment