Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, August 8, 2013

HUDUMA ZITOLEWAZO NA WAKALA WA HUDUMA ZA AJIRA TANZANIA (TaESA)

Picture 246 ba95b
Msemaji wa Wakala wa Huduma za Ajira Bw. Peter Ugata (Kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu jitihada zinazofanywa na wakala hao katika kuhakikisha wanakabiliana na changamoto za ajira nchini, katika mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, KUSHOTO ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa.



Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) ulianzishwa kwa Sheria Na. 30 ya mwaka 1997 (kama iliyorekebishwa mwaka 2009) na kuzinduliwa rasmi tarehe 16 June, 2008 kufuatia Tamko la Serilkali Na.189 la mwaka 2008. TaESA ilianza rasmi utekelezaji wa shughuli zake tarehe 1 Julai, 2008 ikichukua nafasi ya kilichokuwa Kituo cha Ajira nchini (Labour Exchange Centre).
Madhumuni ya kuanzishwa kwa Wakala huu ni katika juhudi za Serikali kuona kuwa utoaji wa Huduma za Ajira kwa umma unakuwa bora zaidi, wenye tija na wenye kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Wakala hutoa huduma zake kwa umma kupitia ofisi zake za kanda zilizopo katika mikoa ya Dar es Salaam (Kanda ya Mashariki na Pwani), Mwanza (Kanda ya Ziwa), Dodoma (Kanda ya Kati) na Arusha (Kanda ya Kaskazini).
Dhima
"Kutoa huduma bora za ajira katika sekta ya utumishi wa umma na binafsi kupitia uunganishwaji watafutakazi, taarifa za soko la ajira kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika Afrika na kwingineko".
Dira
"Kuwa Wakala bora, imara na endelevu katika utoaji huduma za ajira katika sekta ya utumishi wa umma na binafsi".
2.0 SHUGHULI ZA WAKALA
- Kuunganisha watafutakazi na waajiri wenye fursa za ajira ndani na nje ya nchi.
- Kuratibu utoaji mafunzo ya ujuzi wa kazi na ushauri wa ajira.
- Kuandaa mipango ya utoaji huduma za ajira kwa waajiri, watafutakazi na wadau wengine.
- Kukusanya, kuchambua na kusambaza taarifa za soko la ajira.
- Kuainisha na kuzitambua Wakala binafsi zinazotoa huduma za ajira
- Kuratibu utoaji mafunzo yenye kulenga kuwapatia ujuzi wa kazi wanafunzi wanaosoma katika shule za sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu.
2.1 UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA WAKALA
Katika kuhakikisha kuwa Wakala unatekeleza Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008; Sheria ya Kukuza Ajira Na. 9 ya mwaka 1999 na katika hatua ya kukidhi matakwa ya Azimio Na. 88 la mwaka 1948 la Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambalo Tanzania imeliridhia, Wakala umeendelea kutekeleza shughuli zake kwa njia zifuatazo:-
2.1.1 Kuwasajili na kuwafanyia usaili wa awali watafutakazi
2.1.2 Kutembelea waajiri ili kubaini fursa za ajira zitakazojazwa na watafutakazi waliosajiliwa na wakala
2.1.3 Kutembelea shule/vyuo ili kuwajengea uwezo wanafunzi ili kubaini hali halisi ya soko la ajira na mahitaji yake.
2.1.4 Kuendesha vipindi vya kuwajengea uwezo watafutakazi ili waweze kumudu ushindani na changamoto za Soko la Ajira.
2.1.5 Kufanya mikutano na wadau ili kupata maoni/mapendekezo yatakayofanikisha utekelezaji wa majukumu ya Wakala.
2.1.6 Kushiriki katika maonesho ya kitaifa na kimataifa kwa lengo la kujitangaza na kufikisha huduma karibu zaidi na wananchi.
2.1.7 Kujitangaza kupitia vyombo vya habari vikiwemo radio, televisheni na magazeti.
2.1.8 Kwa kutumia Tovuti ya Wakala katika kutoa taarifa na kupata maoni ya wadau na umma kwa ujumla.
2.1.9 Kwa kutumia ofisi zake za Kanda.
3.0 MAFANIKIO YA WAKALA
Tangu kuanzishwa kwake hadi Juni, 2013 Wakala umefanikiwa katika maeneo yafuatayo:-
3.1 Kuanzisha Ofisi za Kanda katika Mikoa ya Dare es Salaam,
Dodoma, Mwanza na Arusha ili kuzifikisha huduma zake karibu na wananchi.
3.2 Wakala umewahudumia jumla ya wateja 13,188 kati yao
Watafutakazi 12,298, waajiri 830 na wakala binafsi 60
3.3 Wakala umeweza kusajili fursa za kazi 2,851 kwa kutembelea Waajiri 830 katika mikoa ya Shinyanga, Kagera,Mara, Mwanza, Singida, Tabora, Iringa, Morogoro, Lindi,Arusha, Kilimanjaro na Mtwara
3.4 Wakala umeendesha vipindi kwa watafutakazi 1,426 kwa lengo la kuwajengea
uwezo watafutakazi ili waweze kuhimili ushindani na
changamoto za soko la ajira.
3.5 Watafuta kazi 8,294 wamepewa ushauri juu ya uchaguzi wa
fani, mafunzo ya kazi zinazostahili kulingana na sifa zao ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajirika.
3.6 Wakala umeainisha Wakala Binafsi 60 zinazotoa huduma za
ajira hapa nchini.
3.7 Kupitia kitengo chake cha kuunganisha watafutakazi na
waajiri nje ya nchi, Wakala umeunganisha watafutakazi 1,959 katika nchi za UAE, Oman, India, Denmark na Saudi Arabia
3.8 Wakala uko katika hatua za awali za kuwa na mfumo wa
kiteknolojia utakawezesha kukusanya na kusambaza taarifa za soko la ajira.
3.9 Wakala umeanzisha tovuti yake www.taesa.go.tz ambayo
imetembelewa na wadau 440,230 ambao wametoa maoni na mapendekezo mbalimbali juu ya huduma zitolewazo na TaESA.
3.10 Wakala umeweka utaratibu madhubuti wa kuratibu na
kusimamia uunganishaji wa Watanzania kwenye soko la ajira nje ya nchi ili Watanzania waweze kupata kazi za staha na kuepukana na biashara haramu ya usafirishaji watu "human trafficking".
4.0 CHANGAMOTO
4.1 Kutokuwa na rasilimali za kutosha kuwezesha kufikia malengo ya Wakala.
4.2 Kutokuwa na fursa za kazi za kutosha ukilinganisha na idadi
ya wahitimu/watafutakazi waliopo katika soko la ajira.
4.3 Watafuta kazi wengi kuwa na matarajio makubwa kuliko hali halisi ya soko la ajira.
4.4 Baadhi ya waajiri na watafutakazi kutotumia huduma za Wakala
5.0 MIKAKATI WA WAKALA KATIKA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO HIZO
Pamoja na changamoto zilizopo wakala umepanga kufanya
yafuatayo:-
5.1 Kuendelea kuwaunganisha watafutakazi na waajiri ndani na
nje ya nchi na kufanya utafiti katika nyanja za upatikanaji
wa fursa za ajira.
5.2 Kukusanya, kuchambua na kusambaza Taarifa za Soko la Ajira.
5.3 Kuendeleza rasilimali watu ili kuongeza tija na ufanisi.
5.4 Kuendelea kuainisha Wakala binafsi zinazotoa huduma za ajira nchini.
6.0 HITIMISHO
Lengo la kuandaa taarifa hii ni kuwajulisha Watanzania na umma kwa ujumla kuhusu huduma zitolewazo na Wakala kwa kuainisha sheria iliyoanzisha, shughuli za Wakala, utekelezaji wa shughuli za Wakala, mafanikio, changamoto na mikakati ya kukukabiliana nazo. Aidha, Wakala unachukua fursa hii kutoa shukrani za dhati kwa kutupatia fursa hii ya kuuelezea Wakala kwenu na Watanzania kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment