Wakati mvutano kati ya Serikali na wadau mbalimbali kuhusu pendekezo la kufutwa kwa tozo ya kodi ya laini za simu ‘Simcard tax’ ya Sh1,000 ukiwa haujapoa, Chama cha Wenye Mabenki nchini (TBA) kimeibuka na kuitupia lawama Serikali kwa kuanzisha kinyemela sheria ya kodi ya kuhamisha fedha kutoka benki. Taarifa iliyotolewa jana na kusainiwa na Mwenyekiti wa TBA, Dk Charles Kimei imesema kuwa Serikali kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2013 (The Financial Act 2013) ilitangaza ongezeko la tozo hiyo ya kodi kwa asilimia 0.15. Kutokana na tozo hizo, gharama za kibenki kwa wateja zitaongezeka na kumlazimisha mteja aliyekuwa anatuma Sh 10 milioni kwa njia ya Mfumo wa Malipo Makubwa na ya Haraka (TISS) kwa gharama ya Sh10,000, sasa atalazimika kutumia Sh25,000 kutuma kiwango hicho cha fedha. Alipoulizwa kwa njia ya simu jana jioni kuhusu tozo hizo Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa aliomba atafutwe baadaye kwa maelezo kuwa yupo katika kikao. Hata hivyo, alipotafutwa tena simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila majibu. Tayari Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imethibitisha kupitishwa kwa sheria hiyo, huku Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka hiyo, Richard Kayombo akilieleza gazeti hili jana kuwa walitoa barua kwa TBA tangu Julai 16, kuwataka kuanza utekelezaji wa sheria hiyo. Sheria hiyo inasema; Kutakuwa na tozo ya kodi kwa fedha zinazohamishwa kupitia benki, taasisi ya fedha au kampuni ya simu kwa tozo ya asilimia 0.15 kwa kiwango cha fedha kinachozidi shilingi 30,000… Tozo hiyo haitahusu uhamishaji wa fedha kutoka benki moja kwenda nyingine, taasisi za fedha, Serikali na shughuli za kibalozi.” TBA inasema, Serikali imeingiza tozo hiyo kinyemela kwenye sheria na kwamba haikuwemo kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha mwaka 2013/2014 wala kwenye mapendekezo ya muswada wa sheria ya fedha, kwamba ilitolewa kama mabadiliko kwenye sheria. Taarifa hiyo inaeleza kuwa iwapo tozo iliyopendekezwa itatumika kama ilivyo, kutakuwa madhara makubwa katika mzunguko wa fedha kwa kuwa asilimia 12 pekee ya watu wote nchini, ndiyo wanaotumia huduma ya benki. Shirikisho hilo lilifafanua kuwa mabenki yanatumia mfumo wa kuhamisha fedha kwa njia ya simu ili kupunguza pengo lililopo baina ya watu wanaotumia benki na wasiotumia huduma hiyo. “Tozo hilo itaongeza ufisadi na changamoto nyingine za kiuendeshaji kwa kuwa zitawapa watu nafasi ya kutafuta njia ya kukwepa kodi hiyo mpya” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. Shirikisho hilo limebainisha kuwa limeshaiandikia barua TRA na Waziri wa Fedha, kuwataka wakutane kuzungumzia suala hilo na kwamba iwapo Serikali haitaondoa tozo hiyo wananchi wajiandae kulipa kodi hiyo mpya.
NAIBU WAZIRI LONDO ASHIRIKI KUPIGA KURA KATIKA KITONGOJI CHA MJI MPYA MIKUMI
-
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika mashariki
anayeshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Lazaro
LONDO (Mb.) amba...
48 minutes ago
No comments:
Post a Comment