skip to main |
skip to sidebar
Klabu 13 zajazwa `mipesa` ya Azam Tv
Hatimaye kampuni ya Azam Media imezikabidhi klabu 13 za Ligi Kuu ya
Tanzania Bara mamilioni yao yote ya awamu ya kwanza ya fedha zinazolipwa
na kampuni hiyo iliyopewa haki ya kuonyesha ‘live’ mechi zote za ligi
kuu kuanzia msimu ujao.
Mgawo
uliotolewa jana ni wa Sh. milioni 25 kwa kila timu, sawa na asilimia 25
ya Sh. milioni 100 ambazo zitalipwa na Azam TV kwa kila klabu ili
kuonyesha mechi zao kwenye televisheni.
Timu hizo 13
zilizopata mgawo wa Sh. milioni 25 ni Simba, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar,
Azam, Coastal Union, Mbeya City, Ashanti, Rhino, JKT Oljoro, JKT Ruvu,
JKT Mgambo, Tanzania Prison na Ruvu Shooting.
Akizungumza na
NIPASHE jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Wallace
Karia, alisema kuwa zoezi la kuziweka fedha hizo katika akaunti za
klabu lilifanyika jana mchana na sasa viongozi wa timu hizo watakuwa
katika nafasi nzuri ya kuendelea na maandalizi.
Karia alisema
kwamba wanaipongeza kampuni hiyo kwa kuanza kutekeleza kivitendo
makubaliano yaliyomo kwenye mkataba wao na wanaamini kuwa kwa kasi hiyo,
hatimaye ushindani utakuwa mkali katika ligi kuu kuanzia msimu ujao.
"Tayari klabu 13 tumeshaziwekea fedha za udhamini wa Azam, leo (jana)
asubuhi walituwekea katika akaunti ya bodi ya ligi na sisi mchana huu
(jana mchana) tumeshazisambaza kwa klabu zote isipokuwa Yanga," alisema
Karia.
Aliongeza kuwa wanazitaka klabu kuzitumia vyema fedha hizo na kukamilisha malengo ya kuendeleza timu.
"Tunajua bado wako katika maandalizi ya kuanzisha televisheni yao
lakini kwa kutangulia kutupa fedha kwetu ni faraja na ndiyo makubaliano
yalivyokuwa kwenye mkataba," aliongeza kiongozi huyo.
Alisema
kwamba awamu ya pili ya fedha za udhamini huo itatolewa kabla ya
kumalizika kwa mzunguko wa kwanza Novemba 3 mwaka huu na kwa msimu mmoja
kila timu itapata Sh. milioni 100.
Alizikumbusha klabu hizo
kuhakikisha kwamba zinakamilisha maandalizi ya msingi ili kushiriki ligi
hiyo na si kuangalia zoezi la usajili wa wachezaji na makocha peke
yake.
"Bima za wachezaji ni suala muhimu lililopo katika kanuni
na msimu huu hatutakubali kuona ubabaishaji unafanyika kama ilivyokuwa
huko nyuma.
Tunataka kuwa na ligi bora, hivyo kila jambo ni lazima lifuatwe ili kufikia maendeleo," aliongeza Karia.
Alisema vilevile kuwa klabu zinatakiwa kushirikiana na wamiliki wa
viwanja ili kurekebisha kasoro zilizopo na endapo hakutakuwa na
marekebisho, timu zitatakiwa kuhama viwanja walivyovichagua.
Chanzo: Nipashe.
No comments:
Post a Comment