DUNIA ni mviringo kama tufe, ndiyo maana wakati wengine wapo mlimani, kuna waliopo bondeni. Wewe unapigwa na jua, yupo ambaye amestarehe kivulini. Ila kwa hakika, hujafa hujaumbika!
Mtoto Nassoro Amiri, 3, (pichani) anateseka jamani. Tangu alipozaliwa, hajawahi kufurahia maisha. Kila nukta kwake ni mateso kwa asilimia 100.
Nassoro, anasumbuliwa na tatizo la uvimbe mkubwa mgongoni ambao unamtesa sana. Vilevile anasumbuliwa na maradhi ya mshipa (henia) ambayo pia yanafanya akose furaha kabisa ya maisha.
Matatizo hayo makubwa mawili, yamemfanya mama wa Nassoro, Hanifa Rashid, ashindwe kufanya kazi nyingine, kwani muda wake wote anautumia kumwangalia mwanaye ambaye anahitaji uangalizi wa hali ya juu.
Kwa uchungu mkubwa, Hanifa anasimulia kuhusu mateso ya mwanaye: “Huyu mwanangu nilimzaa kwa njia ya oparesheni mwaka 2010 katika Hospitali ya Misheni, Mchukwi, Rufiji.
“Baada ya kumzaa tu, aligundulika ana uvimbe mkubwa mgongoni. Niliumia sana baada ya kumuona mtoto wangu yuko katika hali hiyo. Sikuwa na jinsi zaidi ya kumshukuru Mungu.
“Baadaye madaktari waliniandikia rufaa kwenda Hospitali ya CCBRT Dar. Nilipofika, nako nikapelekwa Muhimbili katika Kitengo cha Tiba ya Mifupa (Moi) ili mtoto afanyiwe upasuaji.
“Kweli upasuaji ulifanyika na baada ya mtoto kupata nafuu kidogo, nilirudi nyumbani kwetu Rufiji ambako muda mfupi tu baadaye, mtoto akagundulika ana henia.
“Tulirudi tena Muhimbili ambako alifanyiwa upasuaji wa henia kisha tukarejea Rufiji. Hatukukaa sana, tukagundua mtoto amepooza kuanzia kiunoni kushuka chini. Kwa kweli niliumia sana, nikajiuliza mbona mitihani kwa mwanangu inaongezeka? Kwa vile nilikuwa na kawaida ya kumpeleka mwanangu Muhimbili kliniki kutokana na tatizo lake la uvimbe ambalo halijaisha, madaktari walipoona amepooza, wakamuwekea mpira ili awe anajisaidia.
“Ule mpira, niliambiwa na madaktari kwamba kila ukiisha ninunue mwingine nimuwekee, uwezo sina, fikiria mume wangu aliamua kuniacha kutokana na matatizo ya huyu mtoto.
“Baada ya kuona mume sina, vilevile ukizingatia kwamba natakiwa kila mwezi nimpeleke mwanangu Muhimbili kliniki, imenibidi nihamie Dar kwa msamaria mwema, kwani uwezo wa kusafiri kila mwezi kutoka Rufiji kuja Dar sina na tatizo lingine limeongezeka, mwanangu ana maambukizi katika njia ya mkojo (UTI). Kuna dawa natakiwa kumpaka ndiyo nimuwekee mpira wa kujisaidia, uwezo sina,” alisema Hanifa.
Kama unajisikia una deni kutokana na mateso ya Nassoro na unataka kumsaidia basi wasiliana na chumba chetu cha habari kwa namba 0754 021 301. Kutoa ni moyo, Mungu ni sababu ya kila kitu, ila ikae akilini mwako kwamba kabla hujafa hujaumbika.
No comments:
Post a Comment