Sultan
Qaboos wa Oman ametoa msaada wa Riali milioni tatu na laki moja za nchi
hiyo kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti mkubwa utakaojengwa katika eneo
la Chuo cha Kiislamu Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Akizungumza
na waandishi wa habari Ofisini kwake Mazizini, Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamhuna amesema ujenzi wa msikiti huo
unatarajiwa kuanza wakati wowote baada ya kutiwa saini makubaliano ya
msingi kati ya Zanzibar na Oman.
Amesema
msikiti huo, pamoja na shughuli za ibada, pia utakuwa ni chimbuko la
kuanzishwa Chuo Kikuu cha Kiislamu Zanzibar na kufanikisha azma ya Rais
wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani karume aliependekeza kujengwa
Chuo Kikuu cha Kiislamu katika eneo hilo alipokifungua chuo hicho.
“Maandaliz
yote ya kujengwa msikiti huu yamekamilika na utakuwa na sehemu ya
kusalia wanawake na wanaume, madarasa sita ya kusomea, chumba cha
Kompyuta na maktaba ya kisasa,” alieleza Waziri wa Elimu.
Akizungumzia
msaada wa masomo ya Elimu ya juu uliotolewa na Mfalme Qaboos (Sultan
Qaboos Academic Fellowship) kupitia Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA)
amesema umeanza kuleta mafanikio na wanafunzi wa kwanza 16 wataanza
kufaidika na msaada huo mwaka huu.
Amesema
wanafunzi tisa watasoma Digree ya tatu na saba watachukua Digree ya
pili katika fani walizoomba na watajiunga kwenye vyuo vikuu vya nchi
tofauti duniani.
Ameongeza
kuwa awali Wazanzibari 170 walipeleka maombi ya kupatiwa nafasi hizo
kupitia mtandao na baada ya mchakato uliofanywa na kamati mbili
zilizoundwa kushughulikia maombi hayo, waliobahatika ni watu 16.
Waziri
Shamhuna amewatoa wasi wasi wananchi kuwa hakukuwa na upendeleo wa
aina yoyote katika kuwapata wanafunzi hao na kila kitu kilifanywa kwa
njia ya mtandao.
“Tumekataa
suala la ujomba au ushangazi katika nafasi hizi, tumetumia mtandao
kuwapata wanafunzi bora na hao ndio waliofaulu kutokana na masomo
waliyoomba na sifa walizanazo,”alisema Shamhuna.
Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Amali amesema hivi sasa wanaendelea kuboresha
masomo ya sekondari na hivi Karibuni watakwenda Oman kuzungumzia suala
hilo ili kupata wanafunzi wengi zaidi wenye sifa za kujiunga kupitia
msaada wa mfalme Qaboos.
“Elimu
ya ya juu haifikiwi mpaka wapatikane wanafunzi bora kutoka sekondari
kwa hiyo ni lazima tujadili vipi tatawaboresha wanafunzi wa Sekondari,”
alisema Waziri wa Elimu.
Amesema
Oman na Zanzibar zimekuwa na mashirikiano makubwa katika nyanja mbali
mbali ikiwemo Elimu na imefadhili Kongamano la Kimataifa litakalo
zungumzia Ustaarabu wa Kiislamu katika nchi za Afrika Mashariki
litakalofanyika kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 4 mwezi ujao Nungwi, Mkoa
wa kaskazini Unguja.
Kongamano
hilo limendaliwa na Taasisi ya Tafiti za Historia na Utamaduni ya
Jumuia ya Nchi za Kiislamu Duniani kwa ushirikiano na Mamalaka ya
kumbukumbu na nyaraka ya Falme ya Oman na wenyeji wa kongamano hilo ni
Wizara ya Elimu Zanzibar ikishirikiana na SUZA.
Shamhuna
ameongeza kuwa Kongamano hilo litahudhuriwa na washiriki 170 kutoka
Nchi 18 zikiwemo za Falme za Kiarabu, Mashariki ya mbali, Afrika
Mashariki na Kati nchi za kusini mwa Afrika, Marekani na Ulaya.
Kongamano
hilo litafunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dkt Ali Mohammmed Shein litafungwa na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKt Mohammed Gharib Bilal tarehe
4/9/2013.
No comments:
Post a Comment