MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha jana
imekataa ombi la hati ya dharura ya dhamana ya mke wa mfanyabiashara
maarufu wa madini mkoani Arusha, Janeth Jackson (32), anayedaiwa kupanga
njama za kumuua mumewe wa ndoa.
Janeth na mshitakiwa wa pili, Novatus
Elias kupitia Wakili wao, Samsoni Rumende waliwasilisha hati hiyo katika
Mahakama Kuu, kuomba dhamana baada ya mahakama ya wilaya ya Arusha
iliyoko Sekei, kuwanyima dhamana.
Mahakama iliwanyima dhamana washitakiwa
hao, kwa maelezo kuwa kufanya hivyo ni kuharibu kesi, kwani kuna
watuhumiwa wengine hawajakamatwa.
Hata hivyo, Jaji Mary Moshi alikataa
kumjumuisha mshitakiwa wa pili katika hati hiyo, kwa maelezo kuwa wakili
hakumjumuisha katika hati.
‘’Katika hati ya dharura, naona jina la
mshitakiwa wa kwanza tu ndiye anayeombewa dhamana, lakini jina la
mshitakiwa wa pili, Elias, haliko hivyo siwezi kusikiliza kwa kuwa ni
kinyume na utaratibu,’’ alisema Jaji Moshi.
Pamoja na hayo, Jaji Moshi alimnyima
dhamana Janeth kwa maelezo kuwa Wakili Rumende amefanya makosa ya
kisheria, kwani alipaswa kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya
wilaya wa kumnyima dhamana mteja wake.
Alisema kuomba hati ya dharura ya kuomba
dhamana, sio utaratibu wa kisheria na kutokana na hali hiyo, alimtaka
wakili huyo kwenda kujipanga upya .
Awali akizungumza mahakamani hapo,
Rumende alimwomba Jaji Moshi kumpa dhamana mteja wake, kwani ana mtoto
mchanga wa miezi mitano.
Rumende alidai kuwa dhamana ni haki ya
msingi ya mteja wake na hawezi kuathiri mwenendo wa kesi na atatii
masharti ya dhamana kwa jamii, inayomzunguka bila ya wasiwasi wowote.
Hoja hizo zilipingwa vikali na Wakili wa
Serikali, Edana Kasala aliyedai kuwa utaratibu umekiukwa na pili
mahakama ya wilaya iko sahihi kuwanyima dhamana washitakiwa hao.
Janeth ambaye ni mkazi wa Moshono,
jijini Arusha pamoja na Novatus Elias, katika kesi hiyo katika mahakama
ya wilaya, wanashitakiwa kwa kula njama ya kutaka kumwua Jackson Manjuru
ambaye ni mume wa Janeth.
Washitakiwa wote wawili pia wanadaiwa
kutenda kosa la kula njama na kutaka kumwua Desderi Sabas, anayeishi
Bukoba mkoani Kagera, ambaye ni mtoto wa nje wa mume huyo.
Washitakiwa wote hawakutakiwa kujibu
lolote mahakamani hapo, kwa sababu Mahakama hiyo kisheria haina mamlaka
ya kusikiliza kesi za mauaji.
source: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment