Katibu wa
Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda
alisafirishwa jana kwa helikopta kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na
kupandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa kujibu mashtaka
yanayomkabili.
Ponda
jana alianza kwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu
asubuhi na kufutiwa mashtaka ya uchochezi yaliyokuwa yakimkabili baada
ya kusomewa mara ya kwanza Agosti 14, mwaka huu akiwa kitandani katika
Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili, baada ya Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea
kumshtaki.
hdg
Alidaiwa kutenda makosa hayo katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano kati ya Juni 2 na Agosti 11 mwaka huu.
Ponda
alifikishwa mahakamani hapo saa 12 asubuhi na baadaye alipandishwa
kizimbani na kufutiwa kesi hiyo, baada ya Wakili Kweka kuwasilisha hati
hiyo ya DPP chini ya Kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa
ya Jinai (CPA).
Hata
hivyo, baada ya kufutiwa mashtaka hayo, aliendelea kushikiliwa na kisha
akachukuliwa na kupelekwa Morogoro ambako pia alisomewa mashtaka ya
uchochezi.
Kuwasili Moro
Sheikh
Ponda aliwasili kwa helikopta ya polisi na kutua kwenye Uwanja wa Gofu,
Morogoro akiwa chini ya ulinzi wa polisi na alipakiwa kwenye gari
maalumu ambalo liliongozana na magari mengine matatu ya polisi huku
ulinzi ukiwa umeimarishwa katika eneo la Mahakama ukiwajumuisha askari
wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), askari wa upelelezi, Usalama wa
Taifa pamoja na mbwa wa polisi na kusababisha shughuli za kazi katika
Mahakama hiyo na ofisi za jirani kusimama kwa muda.
Baada ya
kufika mahakamani saa tano asubuhi, magari yalisimama kwa takriban
dakika 30 kabla ya kumtoa na kumwongoza kwenye Mahakama ya wazi ambayo
tayari ilikuwa umejaa watu.
Baada ya
kumalizika kusomwa kwa kesi hiyo, msafara uleule ulimrejesha Uwanja wa
Gofu saa sita mchana na kupandishwa kwenye helikopta kurejea Dar es
Salaam.
Mahakamani Morogoro
Ponda
alisafirishwa kwa helikopta ya polisi hadi Morogoro na kufikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi akiwa chini ya ulinzi mkali.Mara
baada ya kumfikisha katika Mahakama hiyo iliyofurika mamia ya waumini na
wafuasi wake, Wakili wa Serikali, Bernard Kongola alimsomea mashtaka
matatu yanayomkabili.
Mbele ya
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate alisema: "Agosti
10, mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro
Ponda Issa Ponda, aliwaambia wafuasi wake.
"Ndugu
Waislamu, msikubali uundwaji wa Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti
kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata ambao ni vibaraka wa CCM na
Serikali na kama watakuja kwenu na watajitambulisha kwamba wao ni Kamati
za Ulinzi na Usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya
msikiti yenu na muwapige sana."
Kongola
alisema kauli hiyo ilikuwa ikiumiza imani za watu wengine na kwamba
hatua hiyo ni kinyume cha agizo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
lililotolewa na Hakimu Victoria Nongwa Mei 9, mwaka huu ikimtaka
kuhubiri amani ndani ya mwaka mmoja na kwenda kinyume na kifungu cha
Sheria namba 124 cha mwaka 2002, shtaka ambalo Ponda alikana.
Katika
shtaka la pili, Ponda anadaiwa Agosti 10 mwaka huu katika eneo la
Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro aliwaambia Waislamu kuwa Serikali
ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia vurugu iliyotokana na gesi kwa
kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi
wake ni Waislamu.
Alisema
Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu
asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa
sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo na kuwa maneno hayo
yaliumiza imani za watu wengine jambo ambalo ni kinyume cha Kifungu cha
Sheria 129 cha mwaka 2002, shtaka ambalo pia alikana.
Shtaka la
tatu linafanana na lile la pili lakini na upande wa mashtaka ulieleza
kuwa maneno hayo yaliumiza imani za watu wengine na kwamba kufanya hivyo
ni kinyume cha Kifungu 390 cha Sheria na Kanuni ya Adhabu namba 35 cha
mwaka 2002, shtaka ambalo Sheikh Ponda alilikana. Baada ya kusomwa kwa
mashtaka yote matatu, wakili wa Serikali aliiambia Mahakama kuwa
upelelezi wa kesi umekamilika na kupanga kesi kuanza kusikilizwa
Septemba 2 mwaka huu. Upande wa utetezi uliomba Mahakama kupanga kuanza
kusikilizwa kwa kesi Agosti 26, mwaka huu.
Hakimu Kabate aliwapa mawakili kujadiliana na baadaye kuomba kesi hiyo ianze kusikilizwa Agosti 28 mwaka huu.
Wakili alalamika
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Wakili wa Ponda, Juma Nassoro alilaani kitendo cha
kuondolewa kwa mteja wake gerezani na kwenda kusomewa mashtaka mapya
Morogoro bila taarifa.
Alidai
kuwa polisi wanaendelea kukiuka taratibu za kumshikilia kiongozi huyo
kutokana na kufanya mambo kinyume na sheria kwa lengo la kutaka waumini
kufanya vurugu ili waendelee kumshikilia kiongozi huyo."Kitendo cha
kumuondoa mteja wangu gerezani na kwenda kumsomea shtaka jingine
Morogoro nimelilaani. Sijalipenda. Polisi hawakuwa na nia nzuri na Ponda
kwa sababu sheria zinajulikana na kila mtu ana haki ya kutetewa,"
alisema Nassoro.
Akizungumzia
kufutiwa kesi Mahakama ya Kisutu, Nassoro alisema Serikali imeamua
kufuta kesi kabla ya kusikilizwa baada ya kuona imeelemewa kwani
alishapeleka maombi ya kuirudisha Mahakama Kuu kutoka Kisutu kutokana na
Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na maombi hayo
yalipewa namba 11/2013.
Msemaji
wa familia, Isihaka Rashidi alisema: "Hawa jamaa wamempeleka Morogoro
kwa siri kwa sababu jana (juzi) tulikwenda Segerea hakukuwa na hizo
taarifa. Tumekuja kushtuka asubuhi baada ya mke wake kwenda kumpelekea
chai na kuambiwa ameondolewa na kupelekwa Morogoro."
Alisema
baada ya kupata taarifa hizo iliwalazimu kuwasiliana na ndugu zao
waliopo Morogoro kwa ajili ya kwenda mahakamani kusikiliza kesi
hiyo:CHANZO MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment