POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
imebaini kuwa chombo kilichodhaniwa kuwa bomu katika Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama hakikuwa bomu,
bali ni kifaa cha Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) cha kuchunguza anga.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Suleman Kova alisema hayo jana alipozungumza na waandishi
wa habari, baada ya kufanya uchunguzi kwa kushirikiana TMA.
"Baada ya kupata taarifa, polisi
walifika eneo la tukio na kukuta kifaa kilicho katika umbo la kasha
kikining'inia kwenye transfoma karibu na Kanisa kikiwa kinawaka taa.
“Katika kasha hilo kulikuwa na maandishi ya kalamu ya wino yaliyosomeka TMA na Airport," alisema Kamanda Kova.
Alisema baada ya uchunguzi wa awali,
polisi walibaini kuwa kifaa hicho si bomu na kuondoka nacho kwa
uchunguzi zaidi. Mtabiri Mwandimizi wa hali ya hewa kutoka TMA,
Augustino Kanemba, alisema kifaa hicho kinaitwa Radio Sound na hutumiwa
na Mamlaka hiyo kufanya utafiti wa hali ya anga za juu.
"Kifaa hiki hurushwa juu kuleta taarifa
ya hali ya anga, kwa kawaida hufungwa puto ili kipae angani na baada ya
kufika juu, puto hupasuka na kutua sehemu yoyote ya Dar es Salaam … hili
si bomu," alisisitiza Kanemba.
Hata hivyo, Kamanda Kova alipongeza
washarika wa Kanisa hilo, kwa kutoa taarifa Polisi na kuomba waendelee
kufanya hivyo wanapoona kitu wasichokielewa.
Akizungumzia mlipuko katika Kanisa la
KKKT, Usharika wa Segerea, Kamanda Kova alisema Polisi Kanda Maalumu Dar
es Salaam, kwa kushirikiana na wataalamu wa fani za ugaidi na matumizi
ya mabomu kutoka makao makuu ya Jeshi hilo, wanafanya upelelezi kubaini
waliohusika na tukio hilo.
Katika tukio hilo la Agosti 24 mwaka huu
saa 8 usiku, waumini wapatao 20 wakiwa wanaendelea na ibada, ghafla
walitokea watu wanne na kuingia kanisani na kutupa chupa ya bia ikiwa na
utambi na mafuta yadhaniwayo kuwa ya taa eneo la madhabau na
kusababisha mlipuko.
Katika hatua nyingine, Polisi imekamata
wahalifu 180 wakiwamo majambazi katika msako ulioendeshwa na Jeshi hilo
ndani ya wiki moja. Pia imekamata bastola mbili, risasi tisa, magunia
mawili ya bangi na magari mawili ya wizi.
SOURCE: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment