Dar es Salaam. Wafuasi wa
Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda
wamepiga kambi katika Gereza la Segerea, Dar es Salaam wakitaka kumwona
bila mafanikio.
Wakizungumza jana nje ya gereza hilo, wafuasi hao
walisema walipofika hapo saa nne asubuhi waliambiwa kwamba tayari ndugu
zake wanne walikwisharuhusiwa kuingia kumwona.
“Tumeambiwa kwamba idadi watu hao inatosha na
kwamba wengine haturuhusiwi kumwona,” alisema mmoja wa wafuasi hao,
Baraka Mohamed na kuongeza: “Tunaendelea kusubiri huruma za askari wa
Magereza labda baadaye wanaweza kuturuhusu kumwona,” alisema.
Wafuasi hao ambao walijaza sehemu kubwa ya eneo la
mapokezi na nje ya gereza hilo walilalamikia kitendo cha askari hao
kutokuwaruhusu kumwona kiongozi wao.
“Nimefika hapa asubuhi na mapema, lakini utaratibu
sikuupenda kwa kweli. Nimezuiwa nami nataka kumwona kiongozi wangu na
si mimi tu tuko wengi hapa,” alisema mfuasi huyo.
Wafuasi hao hawakukata tamaa kwani licha ya
kuzuiwa waliamua kukaa jirani na lango la gereza na wengine kusimama
vikundi vikundi wakijadiliana namna ya kupata nafasi ya kumwona. Sheikh
Ponda ambaye alikuwa amelazwa katika Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili
(Moi) alipelekwa katika gereza hilo Alhamisi iliyopita.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kusomewa shtaka la
uchochezi akiwa kitandani akidaiwa kutenda kosa hilo katika maeneo
mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya Juni 2 hadi Agosti
11 mwaka huu.
Kwa nini walizuiwa?
Ofisa Habari wa Jeshi la Magereza, Deodatus
Kizinja alisema jana kuwa kisheria ni watu wawili katika kipindi cha
wiki nne wanaoruhusiwa kumwona kila mahabusu.
Hata hivyo, alisema kwa kuzingatia sababu
mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na wananchi, wamekuwa wakiruhusu
idadi zaidi kila inapobidi.
“Kwa watu maarufu kama Ponda, Jeshi la Magereza
linakuwa makini kudhibiti umati wa watu wanaotaka kumwona mahabusu kwa
sababu hatuwezi kufahamu kama watu wote wana nia njema au la,” alisema
Kizinja na kusisitiza kuwa ndugu zake wanne ambao walishaingia kumwona
wanatosha.
No comments:
Post a Comment