HUWEZI kutawala miili ya watu ukaacha mioyo yao. Ndiyo, mjumbe hauawi, ni kauli ya hekima ya tangu enzi za wahenga wetu.
Leo ni mwaka mmoja tangu mwandishi
wa habari na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wandishi wa Habari
mkoani Iringa,Daud Mwangosi kuawa.
Ilikuwa ni Jumapili ya Septemba 2,
2012. Hakika, siku ile itabaki katika kumbukumbu za Watanzania kwa
mamilioni. Ni kwa kufikiwa na taarifa za kutisha za mauaji ya mwandishi
wa habari. Haya yanaingia katika historia kuwa ni mauaji ya kwanza kwa
mwandishi wa habari kufanyika hadharani tangu nchi hii ipate
Uhuru. Wengi watakuja kukumbuka walikuwa wapi na walifanya nini siku
walipopata taarifa hizo za kutisha. Binafsi, taarifa ile ya mauaji
ya Daud Mwangosi siku ile ya Jumapili ya huzuni kwa Taifa ilinikuta
nikiwa Iringa Mjini. N umbali wa mwendo wa saa moja kwa gari kufika
eneo la tukio, Nyololo, Mufindi.
Jioni ile nilikuwa nikifundisha
soka ya watoto. Mara baada ya kupata taarifa zile kwa simu, nilisitisha
mazoezi yale ya watoto. Nikawapa taarifa zile. Nilipowaambia kuwa
nimepata taarifa sasa hivi kuwa mwandishi wa habari ameuawa Mafinga,
mtoto mmoja akaniangalia na kuniuliza; “ Kwanini?”
Ndiyo, swali la mtoto yule ndilo umma wa Watanzania unapaswa uendelee kujiuliza hata leo; KWA NINI?
Mwandishi wa habari ni mjumbe
katika jamii. Anapokuwa akifanya kazi yake hapaswi kuwa na hofu ya
kudhuriwa kwa kukusudia na waliopata mafunzo ya kutumia silaha. Ndivyo
ilivyo kwa watumishi wa Msalaba Mwekundu, wanapokuwa kazini kwenye
maeneo hata ya vita.
Askari asiyejua kutofautisha kati
ya mwanahabari aliyeshika kamera, mtu wa Msalaba Mwekundu aliyeshika
mkoba wa Huduma ya Kwanza na raia anayefanya vurugu au adui aliyeshika
silaha vitani, huyo hawezi kuwa ni askari makini.
Na hakika, kama Taifa, tunafanya
makosa kuamini, kuwa nchi yetu ni ya amani kwa vile wananchi wetu
hawagombani. Kama watu hawagombani kuwa na maana nchi ni ya
amani yaweza kuwa tafsiri potofu ya maana nzima ya amani. Maana, kama
watu hawagombani mahali pasipo na haki, usawa na uadilifu wa viongozi;
mahali palipojaa dhuluma,unyanyasaji na maovu mengine wanayotendewa au
wanaotendeana wanajamii, basi, amani hiyo itakuwa ni ya muda tu.
Maana, kwa watu wenye kuishi kwenye mazingira hayo bila kugombana wala kutokea uvunjifu wa amani, hiyo itakuwa na maana ifuatayo; ama watu hao hawaelewi kuwa wanaishi katika mazingira hayo ya dhuluma na maovu mengine wanayotendewa au kutendeana, au wamejawa na hofu.
Hivyo basi, kwa hilo la mwisho,
itakuwa ni amani iliyojengeka katika misingi ya hofu. Na hofu hiyo
haiwezi kuwa ya kudumu. Kuna siku mwanadamu hufikia ukomo wa kuhofia.
Ukimwandama sana mjusi, mwisho hugeuka nyoka! Ndipo hapo tunapoona nchi
zinalipuka na watu kuchinjana.
Hii ni nchi yetu. Katika tofauti
zetu hizi za kiitikadi tusifike mahali tukashindwa kuongea kama
Watanzania kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania. Kuna umma uliopo na
unaokuja. Umma unaotegemea sana busara katika uongozi wetu. Tuanze sasa
kujenga utamaduni wa kuitumikia nchi yetu kwa kufanya na kuamua yale
yenye maslahi kwa Tanzania. Hivi vyama vya siasa vipo leo na kesho
havipo. Vinakuja na kuondoka, lakini Tanzania kama nchi itakuwapo daima.
Tusifike mahali tukabaki
tunawaangalia wanasiasa wetu, kwa maslahi yao binafsi, ya makundi yao na
vyama vyao, wakashinikiza au kuelekeza yale yenye kuchochea machafuko
makubwa ya kijamii. Ni wajibu wa viongozi wa kisiasa kutanguliza busara
katika kila maamuzi wayafanyao.
Na tunafanyaje pale tunapowaona
viongozi wa kisiasa na watendaji wakifanya maamuzi yasiyo na busara na
kusababisha Watanzania wenzetu kupoteza uhai na hata kuchochea
machafuko?
Jibu; Kama Watanzania wazawa na wazalendo wa nchi hii, tuna wajibu wa kuyalaani matendo yao maovu.
Na katika nchi zetu hizi, ni kazi
rahisi sana kuanzisha vurugu na kujenga mazingira ya chuki na uhasama,
lakini, ni kazi kubwa sana kumaliza vurugu na kuondosha mazingira hayo
ya chuki na uhasama. Na nchi yetu kamwe haiwezi kupiga hatua za maana za
maendeleo katikati ya mazingira ya vurugu, chuki na uhasama, uwe wa
vyama vya siasa au wanajamii.
Kihistoria, Watanzania tumeishi
kwa amani na upendo bila kuwa na chuki na uhasama miongoni mwetu
unaotokana na tofauti zetu za kidini na kikabila. Tunaziona sasa, dalili
za baadhi ya wanasiasa, kwa malengo ya kisiasa, kutaka kupandikiza
miongoni mwetu uhasama na chuki kwa kutumia tofauti zetu za kidini na
kikabila, tofauti zetu za kiitikadi. Wanafanya hivyo mara ile
wanaposhindwa kujenga hoja za kisiasa kwenye majukwaa ya kisiasa. Hawa
ni watu hatari sana kwa maslahi ya taifa letu.
Katika nchi zetu hizi, ni
wanasiasa wa aina hii ambao, katika kufanikisha malengo yao, huwa
tayari hata kuwalipa vijana wasio na ajira na kuwavutisha bangi ili
washiriki vurugu za kisiasa, kidini na kikabila. Tumeyaona hayo
Liberia, Ivory Coast na hata katika nchi jirani na kwetu.
Tusipokuwa makini, yako karibu kupisha hodi kwenye nchi yetu, kama si tayari kuwa yameshaingia ndani ya nchi yetu.
Hii ni nchi yetu. Tutafanya makosa
makubwa kuwaachia viongozi wa kisiasa pekee, jukumu la kulinda maslahi
ya nchi yetu. Tunapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate Uhuru. Dunia
imebadilika, na nchi yetu inapitia kwenye kipindi cha mabadiliko.
Hakuna mtu au chama cha siasa kinachoweza kuyazuia mabadiliko haya.
Kufanya hivyo ni kutuletea machafuko na kuvunja amani yetu. Tuna jukumu
la kufanya tunayoweza, na kwa kutanguliza busara, kuipitisha salama nchi
yetu katika kipindi hiki cha mabadiliko.
Maana, tukiingia kwenye machafuko,
basi, hakutakuwa na mshindi, maana, sote tutashindwa. Na kifo cha Daudi
Mwangosi kinatutaka tuyatafakari haya.
Maggid,
Iringa.
No comments:
Post a Comment