Mama mzazi wa Ngwea, Denisia Mangweha (kulia) akiwa na aliyekuwa mchumba wa mwanaye aitwaye Misheily.
Habari za kiuchunguzi kutoka ndani ya familia zimeeleza kuwa
ukiachilia mbali cheti cha kifo cha Ngwea walichopewa siku kadhaa baada
ya mazishi ya mtoto wao, hawajawahi kuelezwa kwa kina juu ya kile
kilichomsababishia mauti au hata mwenendo wa kesi au uchunguzi wa tukio
hilo.Ilidaiwa kuwa mara kadhaa familia hiyo ilikutana katika vikao vya ndani na kukubaliana kulifuatilia suala hilo katika Ubalozi wa Afrika Kusini jijini Dar. Huko walikumbana na vizingiti kwa maelezo imekataliwa kutolewa nchini humo.
Ilisemekana kuwa ndugu hao walipokwenda mara ya mwisho ubalozini hapo waliambiwa waandike barua ya kuomba kujua kinachoendelea ikiwa ni pamoja na ishu ya kama kuna kesi katika tukio hilo.
Habari nyingine zilidai kuwa huenda ripoti hiyo ilikwama sehemu au uchunguzi haujakamilika.
Baada ya kujishibisha na data hizo, gazeti hili lilisaga lami hadi Mazimbu Road, Kihonda mjini hapa nyumbani kwa mama Ngwea, Denisia Mangweha ili kupata undani wa habari hiyo.
Juu ya suala hilo mama Ngwea alisema: “Ukweli kama familia hatujakabidhiwa ripoti wala hatujui kinachoendelea.
“Mwezi uliopita tulikaa kikao kwa baba mdogo wa Albert (Ngwea), David Mangweha nyumbani kwake Mbezi jijini Dar ambapo tuliamua kufuatilia mambo hayo.
“Pia ni kweli tulimtuma kaka yake lakini walituambia kama familia tuandike barua ya kuomba ripoti na masuala mengine na tutume mtu kutoka ndani ya familia aende Afrika Kusini kwani hata wao hawajaipata, jambo ambalo ndiyo tunaendela nalo.
Wakati hayo yakiendelea, wiki iliyopita mchumba wa Ngwea alifika nyumbani hapo akitokea Dar ambapo alisababisha vilio upya huku akieleza jinsi ambavyo amekuwa akilia kila kukicha na kushindwa kuishi bila Ngwea.
Hadi gazeti hili linaanua virago nyumbani hapo mchumba huyo wa Ngwea alikuwa akiendelea kumfariji mama mkwe wake kwa maelezo kuwa anahisi kuendelea kuishi Dar bila msanii huyo kutamshinda.
Ngwea alifariki dunia ghafla Juni 28, mwaka huu huko Afrika Kusini ambapo hali leo wengi wamekuwa wakitaka kujua ukweli juu ya chanzo cha kifo chake.
GPL
No comments:
Post a Comment