Kiongozi mwandamizi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya
Kiislamu,Sheikh Khalid Azzan Hamdan amelazwa katika Hospitali ya Mnazi
Mmoja akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza na polisi kuanzia
Septemba Mosi mjini hapa imefahamika.
Akizungumza na Mwananchi Kamishna wa Chuo cha
Mafunzo Zanzibar (Magereza), Khalifa Hassan alisema Azzan aliwahi
kuishiwa nguvu za miguu mara mbili akiwa katika mahabusu ya Gereza la
Kinuai,Mkoa wa Mjini Magharibi kisiwani Unguja.
Hassan alisema,kufuatia hali hiyo, magereza
waliamua kumpelekea katika hospitali hiyo ya Mnazi Mmoja na kuamriwa
alazwe kwa uchunguzi zaidi na matibabu kufuatia afya yake kuzorota
ghafla. Alisema, watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na kesi ya uharibifu
wa mali na kuhatarisha usalama wa Taifa mbali na Azzan, wanaendelea
vizuri na wako katika afya njema ambapo jana walifikishwa mahakamani
bila ya mshtakiwa mwenzao huyo kuwapo.
Wakili wa washtakiwa hao, Abdallah Juma alisema
baada ya kupokea taarifa za mteja wake kuwa mgonjwa, aliamua kumjulia
hali akiwa hospitali, lakini askari walioimarisha ulinzi katika chumba
cha wagonjwa wa mahabusu na wafungwa walisema hawawezi kumruhusu bila ya
kupewa kibali cha uongozi wa magereza Zanzibar.
Hata hivyo, Wakili Abdallah alisema, mteja wake
Azzan anasumbuliwa na matatizo katika kibofu cha mkojo kutokana na kuwa
na vijiwe ambapo alitakiwa kutibiwa nchini India na Afrika Kusini.
Katibu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja,Omar Abadllah
Ali alisema kwamba tayari daktari anayemshughulikia ameshachukua vipimo
muhimu na anaendelea kufanya vipimo maalumu kwa kutumia mashine ya
picha.
Hata hivyo alisema ni mapema kuyazungumzia maradhi
yanayomsumbua mtuhumiwa huyo, lakini alikiri na kusema amelezwa katika
chumba maalumu hospitalini hapo.
No comments:
Post a Comment