MEYA
wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani, anadaiwa kukesha ofisini na
baadhi ya watendaji wake, hatua inayoibua taharuki kwa wananchi kuwa
huenda anabadili nyaraka kabla ya kukaguliwa.
Hali
hiyo imekuja zikiwa ni siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete
kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua
miradi inayotek
elezwa na meya huyo baada ya madiwani kudai ina harufu ya kifisadi.
Kwa
mujibu wa vyanzo vyetu kutoka mjini Bukoba, Amani alionekana kwa siku
mbili na baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo ofisini usiku wa
manane, hatua iliyowalazimu baadhi ya wananchi kuhoji ni kazi gani
zinafanyika usiku kucha hasa wakati huu wa mgogoro.
Kabla
viongozi hao hawajafika mkoani humo, Amani alimrejesha kazini katibu
muhtasi wake aliyekuwa amestaafu ili aweke mambo sawa.
Tayari
baadhi ya madiwani wanaompinga meya huo, wamemtaka akae kando ili
kupisha wataalamu wa CAG kufanya kazi yao bila kuingiliwa.
Wakizungumzia
kitendo hicho cha meya kujifungia ofisini usiku na baadhi ya watendaji
kabla ya CAG kuanza ukaguzi, walisema kinatia mashaka na kuitaka
serikali imchukulie hatua haraka kabla ya kupoteza ushahidi mhimu.
“Tunatoa
tahadhari mapema kwa serikali na CCM wajue kuwa mtuhumiwa ameanza
kujihami kwa kukesha ofisini na watendaji wake, hili si jambo la kawaida
CAG atapaswa kuwa makini zaidi,” walisema madiwani hao.
Amani hakupatikana kujibu tuhuma hizo kwani simu yake ya kiganjani haikupatikana hewani alipotafutwa.
Katika
kumaliza mgogoro wa umeya mjini Bukoba, Kamati Kuu ya CCM (CC)
ilitengua uamuzi wa kuwafukuza madiwani wanane wa manispaa hiyo, ambapo
chama kilidai kuwa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kagera iliyokuwa
imewafukuza ilikiuka katiba.
Kamati
Kuu chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete ilimwagiza CAG kwenda
mjini Bukoba wiki hii ili kukagua tuhuma hizo dhidi ya meya na kisha
ripoti hiyo kuwasilishwa kwenye baraza ka madiwani ili hatua zaidi
zichukuliwe ikithibitika alifanya ufisadi.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho cha CC kilichoketi hivi karibuni mjini
Dodoma zilisema kuwa Kikwete alikiri timu iliyoundwa na Waziri Mkuu
kuchunguza mgogoro huo kuwa ilibaini mianya ya ufisadi katika manispaa
hiyo.
“Rais
alisema hawezi kumfukuza meya kwa vile mamlaka hayo yako kwa madiwani
waliomchagua, hivyo aliagiza CAG aende Bukoba kuchunguza tuhuma hizo
halafu ripoti iwasilishwe kwenye baraza la madiwani hatua zichukuliwe,”
alisema mtoa taarifa.
Hatima ya meya itategemea kitakachokuwa kimegunduliwa na CAG na kuwekwa katika ripoti hiyo.
“Baada ya hapo madiwani wanaweza kufanya lolote wanalotaka.
“Kama ni kumfukuza meya au la wataamua wao, kwa maana sasa watakuwa na vielelezo halisi mbele yao,” kilisema chanzo hicho.
Madiwani
hao wanane waliorejeshwa na kata zao kwenye mabano ni Richard Gaspar
(Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye
pia ni Naibu Meya (Buhembe), Yusuf Ngaiza.
Wengine
ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga),
Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro) na Dauda
Karumuna (Ijuganyondo).
Vile
vile, Rais aliwataka meya na mbunge wafanye jitihada za kupatana na
kufanya kazi pamoja kama ilivyokuwa zamani; hata wakitaka kutumia
viongozi wa dini au wa kisiasa.
Katika
hali inayoonyesha kuwa hoja ya ufisadi ndiyo ilikuwa kiini cha uamuzi
wa CC kutofukuza madiwani, iliamuliwa pia viwanja 800 vilivyokuwa na
mgogoro, warudishiwe wananchi waliokuwa wanavimiliki na wasitozwe hata
senti tano.
Madiwani
hao wamekuwa wanamlalamikia meya kuwa ameiingiza manispaa katika
ufisadi kwenye miradi kadhaa. Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000
unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhamana ya
Uwekezaji (UTT) ambao haukufuata taratibu na wananchi hawakushirikishwa
ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko.
Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani.
Vilevile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90 lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka.
Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi ya kiasi cha sh milioni 134 za ujenzi wa kituo cha mabasi.
Kwa
mujibu wa kanuni za manispaa hiyo yenye madiwani 24, watatu wa CUF,
wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM, ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa
meya, ni lazima robo tatu ya madiwani yaani 16, wapige kura ya kuunga
mkono hoja hiyo. TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment