Picha 1
Mhandisi Mkazi Eng. Peter Gibson (aliyenyoosha mkono) kutoka Kampuni ya Nicholas O’ Dwyer & Partner akimpatia maelezo Waziri wa Ujenzi Mhe. John Pombe Magufuli, kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa barabara ya Mbeya – Chunya. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Abbas Kandoro.
Picha 2
Waziri Wa Ujenzi Mhe. John Pombe Magufuli (katikati aliyeinama) akiangalia mamendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mbeya – Chunya. Kushoto kwa Waziri Magufuli ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Abbas Kandoro.
Picha 3
Waziri Wa Ujenzi Mhe. John Pombe Magufuli (aliyetangulia) akikagua mamendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mbeya – Chunya. Nyuma ya Waziri Magufuli ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Abbas Kandolo.
Picha 4
Mhandisi Mkazi Eng. Peter Gibson (kushoto) kutoka Kampuni ya Nicholas O’ Dwyer & Partner akimpatia maelezo Waziri wa Ujenzi Mhe. John Pombe Magufuli, kuhusu uwekaji wa lami katika barabara ya Mbeya – Chunya sehemu kati ya Lwanjilo na Chunya.
Mkandarasi aliyekuwa amepewa kazi ya kujenga barabara ya kuanzia Mbeya mjini hadi Lwanjilo kwa kiwango cha lami anatakiwa kuilipa Serikali ya Tanzania Shilingi bilioni 16 baada ya kushindwa kesi. Kampuni ya Kundan Singh ya kutoka Kenya iliachakazi za ujenzi kinyume na mkataba na kukimbilia mahakamani ambako imeshindwa na kutakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha. 
Wananchi wa Chunya walijulishwa uamuzi huo na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akiongea katika mkutano wa hadhara mjini Chunya. “Baada ya mradi huu kusimama kwa muda mrefu kusubiri maamuzi ya mahakama hatimaye mradi huu sasa unaendelea na mkandarasi aliyetupeleka mahakamani ameadhibiwa kutulipa shilingi bilioni 16” alibainisha Mheshimiwa Magufuli.
 
Wizara ya Ujenzi inaendelea kutekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kati ya mji wa Mbeya na Chunya kupitia Lwanjilo. Mradi huu umegawanywa katika sehemu mbili ukianzia Mbeya mjini hadi Lwanjilo yenye urefu wa kilometa 36 na sehemu ya pili inaanzia Lwanjilo hadi Chunya pia ikiwa na urefu wa kilometa 36.
 
Mheshimiwa Magufuli aliendelea kufafanua kuwa tayari kuanzia mwezi Desemba 2010, mkandarasi mpya alikwishapatikana na atakamilisha kazi ambazo ziliachwa na mkandarasi wa awali ambaye aliingia mkataba mwaka 2007 na kisimamisha kazi mwaka 2009. Kampuni ya China Communication Construction Company (CCCC) imeshinda zabuni ya kumalizia ujenzi wa sehemu hii ya kwanza kutoka Mbeya mjini hadi Lwanjilo kwa gharama ya Shilingi bilioni 55.4. Mkandarasi huyu baada ya kuwa ameongezewa muda kutokana na mabadiliko ya viwango vya kazi sasa anatakiwa awe amekamilisha mradi huu kabla ya mwezi Desemba 2014.
 
Akizungumzia sehemu ya pili ya mradi huo ambayo inaanzia eneo la Lwanjilo hadi Chunya, inayojengwa na  Kampuni hiyo hiyo ya China Communication Construction Company (CCCC), Mheshimiwa Magufuli alimtaka mkandarasi kuwa amekamilisha kazi zote ifikapo mwezi Aprili mwaka 2014 kama mkataba unavyomuelekeza. Sehemu hii inajengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 40.2.
Kuchelewa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa barabara kati ya Mbeya na Chunya kumekuwa kukilalamikiwa kwa kipindi kirefu. Hivyo kupatikana kwa mkandarasi wa kumalizia kazi kwa sehemu ya kwanza kumeleta faraja kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo ambao wengi wao waliitikia vyema wito wa kubomoa majengo yao yaliyo ndani ya hifadhi ya barabara ili kupisha ujenzi mradi huo.