THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
Fax: 255-22-2113425 |
PRESIDENT’S
OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O.
BOX 9120,
DAR
ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Hakuna
uporaji wa ardhi ya wakulima wadogo unaofanywa na Serikali – JK
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hakuna uporaji wowote
wa ardhi unaofanywa na Serikali yake dhidi ya ardhi ya wananchi na hasa
wakulima wadogo.
Aidha, Rais Kikwete amesema Serikali
ya Tanzania haiwezi kupora ardhi ya wananchi na hasa wakulima wadogo kwa sababu
sera za kilimo za Serikali zinalenga kumlinda mkulima mdogo na kumwezesha
kujikomboa kutoka kwenye umasikini.
Rais Kikwete alitoa msimamo huo, kwa
mara nyingine tena, mwishoni mwa wiki wakati alipozungumza na wana-jumuia ya
Chuo Kikuu cha Guelph cha Toronto, baada ya kuwa ametunukiwa Shahada ya Uzamivu
ya Heshima ya Sheria na Chuo hicho maarufu cha Canada.
Katika hotuba yake ya kupokea na
kukubali shahada hiyo, Rais Kikwete ambaye alizungumzia maendeleo na changamoto
za kilimo katika Afrika alisema kuwa kamwe Serikali ya Tanzania haiwezi kupora
ardhi ya wakulima wadogo wadogo kwa sababu sera ya Serikali katika mipango yote
mikubwa ya kilimo ni kumlinda na kumtetea mkulima mdogo.
“Hakuna uporaji wa ardhi
unaofanywa na Serikali katika Tanzania kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Uporaji wa ardhi ya mkulima mdogo hauwezi kutokea katika Tanzania kwa sababu
sera za Serikali ni kuhakikisha kuwa mkulima mdogo anakuwa mtu wa kwanza
kunufaika na kufaidika na sera za kilimo za Serikali,” alisema
Rais Kikwete na kuongeza:
“Mkulima mdogo yuko katikati ya
mipango na sera za Serikali, na kwa kweli ndiye mtu muhimu zaidi katika mipango
ya kilimo ya Serikali. Kazi ya wakulima
wakubwa ambao tunawakaribisha kuwekeza katika Tanzania ni kuunga mkono shughuli
za kilimo za wakulima wadogo kwa maana kweli kweli ya uwezeshaji.”
Rais Kikwete amesema kuwa kwa kadri
Serikali inavyokaribisha wakulima wakubwa kuwekeza katika kilimo na uchumi wa
Tanzania, ni dhahiri kuwa Serikali itaendelea kuwalinda na kuwatetea wakulima
wadogo ambao watashirikiana na wakulima wakubwa katika kuboresha kilimo cha
Tanzania.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment