Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, October 22, 2013

MADUDU MUHIMBILI YAENDELEA KUFUMULIWA, HAYA NI MAPYA KABISA. SOMA HAPA


Na Mwandishi Wetu

HUDUMA za afya nchini Tanzania ni wasiwasi jumlisha majanga, wapo madaktari wasio waaminifu wanaocheza na maisha ya wagonjwa, miili ya Watanzania ikichokonolewa na kupasuliwa bila sababu.
Kitengo cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) cha gazeti hili, kilipata malalamiko kwamba kwenye hospitali nyingi binafsi, wapo wanaopewa magonjwa ambayo hawana ili wapunwe pesa bure. OFM kilipofanyia kazi tatizo hilo, kilijiridhisha pasipo chembe ya shaka kwamba mchezo huo upo na umeenea kwa kiwango kikubwa, kwani hata mwandishi wetu aliyejifanya mgonjwa ili kubaini ‘uhuni’ huo, nusura apasuliwe tumbo.
Awali, mama wa Kitanzania, Mary-Stella Maulid alitoa malalamiko yake OFM: “Sikuwa na tatizo la appendix (appendicitis au kidole tumbo), pale … (anataja jina la hospitali moja binafsi Dar es Salaam), waliniambia nina appendix.
“Waliniambia natakiwa kufanyiwa oparesheni haraka. Nilimpigia simu mume wangu, akaja pale hospitali, akanipeleka Muhimbili (hospitali ya taifa), alisema haziamini hospitali binafsi kwa oparesheni.
“Pale Muhimbili nikapimwa tena lakini majibu yalipotoka yalionesha sikuwa na appendix, isipokuwa nilikuwa na matatizo katika mfuko wa uzazi, nikapelekwa kwa mtaalamu wa mambo ya uzazi (gynecologist) ambaye alinisaidia sana.  

OFM KAZINI
Oktoba 16, mwaka huu, OFM ilimtuma mwandishi wa kike kwenda katika hospitali iliyotajwa na Mary-Stella ili kujiridhisha, hali ilikuwa hivi;
Mwandishi akijifanya anaumwa sana, alikuwa akitembea kwa kuinama, akilalamikia maumivu ya tumbo.
Saa 4:45 asubuhi alifika hospitalini hapo, akapokelewa na muuguzi mwanamke mwenye umri wa makamo ambaye alimsaidia kumpeleka mapokezi ambako rekodi zake ziliandikwa kisha akapewa kadi yenye namba ya faili lake.
Baada ya hatua hiyo, mgonjwa-mwandishi alisaidiwa kupelekwa kwenye chumba cha daktari ambako baada ya kujieleza, daktari aliagiza akafanyiwe kipimo cha Ultrasound ambacho gharama yake ni shilingi 30,000 kwa bei ya hospitalini hapo.
Kabla ya kuingia chumba cha ultrasound, mwandishi-mgonjwa, alitakiwa kunywa maji kiasi kisichopungua lita moja, baada ya kutekeleza hilo, aliingizwa kwenye kipimo.

UTANI UKAANZA
Majibu ya ultrasound katika hospitali hiyo, yalionesha kwamba mwandishi wetu hana tatizo la appendix lakini daktari akasema: “Utakuwa na tatizo la appendix, ultrasound haioneshi lakini ngoja nikupime zaidi.”
Daktari huyo (jina linahifadhiwa) akaanza kufanya kazi ‘manyuali’, akimshika mwandishi-mgonjwa kwa mikono, akipapasa sehemu ya tumbo kwa chini kisha akaibuka na jibu: “Ni appendix kabisa, inabidi tukufanyie oparesheni.”
Aidha, daktari alimtaka mwandishi-mgonjwa atoe shilingi 600,000 ili afanyiwe oparesheni ya kuondoa kidole tumbo.
Hata hivyo, mwandishi-mgonjwa alisema hana fedha, kwa hiyo akaomba apewe muda na angerudi siku iliyofuata ambapo daktari akiwa na macho makavu, alimruhusu.

MWANDISHI MPAKA MUHIMBILI
Kwa mtindo uleule, mwandishi wetu akijifanya hawezi kutembea vizuri, alikwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili, Oktoba 17, mwaka huu na kufanikiwa kuonana na daktari (jina kapuni).
Daktari huyo baada ya kumsikiliza mgonjwa, alimwambia arudi Oktoba 28, mwaka huu (yaani siku 11 baadaye) ndipo atafanyiwa ultrasound.
Katika cheti cha mwandishi wetu, daktari alimwambia kuwa siku hiyo arudi na maji lita moja, tishu (makaratasi) na afike hospitali saa 2.00 asubuhi.

MWANDISHI AKUNA KICHWA
Majibu ya daktari Muhimbili yalimfanya ajiulize: “Mtu unaumwa tumbo hata kutembea huwezi, unaambiwa urudi nyumbani mpaka Oktoba 28, yaani siku 11 baadaye, je, appendix ikipasuka nikifa?”
Mwandishi aliwaza na kuwazua kisha akaenda Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (Moi) ambako alipokelewa na kupimwa ultrasound chapchapu kwa gharama ya shilingi 40,000.
Majibu ya Moi kama yanavyoonekana ukurasa wa kwanza, ilibainika hana appendix na daktari alishauri afanyiwe CT Scan ili kama kuna tatizo lingine tumboni lionekane.

NINI CHA KUJIFUNZA?
Hali ni mbaya nchini hususan kwenye Jiji la Dar es Salaam kwa sasa, ni wazi kwamba kama Mtanzania asipokuwa mwangalifu, anaweza kufanyiwa oparesheni bila sababu ili mradi  watu wapate pesa!
Uchunguzi wetu umebaini kuwa wetu wengi katika hospitali binafsi wanaingiwa na tamaa mbaya ya fedha, kiasi cha kucheza na maisha ya watu.
“Wengi wameshafanyiwa oparesheni wakati haikuhitajika wafanyiwe. Mtu anachanwa tumbo halafu anashonwa, anaambiwa amekatwa appendix wakati siyo kweli, kuna utapeli mwingi katika baadhi ya hospitali binafsi,” alisema Mary-Stella.
Wakati Watanzania wakitendewa hayo, hali halisi inaonesha kwamba serikali yao haijui chochote.
Uchunguzi zaidi unaonesha kuwa hospitali binafsi zimekosa udhibiti kiasi kwamba zinachaji bei kubwa utadhani huduma za afya ni anasa na siyo mahitaji ya  lazima kwa binadamu.
Imebainika kuwa katika baadhi ya hospitali binafsi, madaktari wake ambao mara nyingi ni waajiriwa wa muda (part-time), wamekuwa wakitumiwa na wamiliki wa hospitali hizo kuwakamua wagonjwa fedha nyingi katika vipimo na matibabu yasiyo ya lazima ili kuingiza fedha.
“Hali ni mbaya sana, imefikia madaktari wanamwandikia mgonjwa vipimo vingi bila sababu lengo likiwa ni kumfanya alipe fedha nyingi ili mradi wao wamechukua sehemu ya malipo hayo,” alisema Anania Bella wa Sinza Mori, Dar es Salaam.
Aidha, OFM imebaini kuwa hata pale daktari anapofahamu mgonjwa wake ana ugonjwa fulani mfano,  malaria, badala ya kupima kwanza damu ili ijulikane, atamwandikia lundo la vipimo kama widal test (typhoid), kipimo kikubwa cha damu  (full blood picture) na mkojo, ili mradi alipe pesa nyingi.
Muuguzi mmoja wa Muhimbili mwenye moyo wa uzalendo (jina tunalo) alisema: “Kinachosikitisha zaidi ni pale mgonjwa anapokuwa anaumwa tumbo, ataandikiwa vipimo vingi vikubwa vya gharama kubwa kama ultrasound ambayo hugharimu shilingi 20,000 mpaka 50,000, CT-Scan shilingi 300,000 na MRI (magnetic resonance imaging) shilingi 450,000.”
Aliongeza kuwa hali huwa mbaya zaidi pale mgonjwa huyo anapolipiwa na bima, kwani gharama hufanywa karibu mara mbili ya bei anayotozwa mgonjwa anayelipa taslimu sababu inayolipa ni serikali.
“Kwa huu mwendo na kama serikali haitafanyia kazi hili, huko mbeleni tunaweza kushuhudia NHIF (Mfuko wa Bima ya Taifa) ikifilisika.
“Tujiulize, kwa nini  kama mgonjwa anaumwa tumbo ili kumpunguzia gharama usimfanyie kwanza ultrasound, usipopata jibu ndipo umfanyie CT-Scan nayo isipoonesha majibu ndipo umfanyie MRI?” anahoji muuguzi huyo.
Taarifa za kusikitisha zaidi zimedai kwamba baadhi ya hospitali jijini zimekuwa zikiwalazimisha wagonjwa kufanyiwa oparesheni hasa za uzazi ambazo hutozwa hadi shilingi milioni mbili ili tu ziingize pesa, wakati wahusika wanaweza kujifungua kwa njia ya kawaida.

MAJANGA MENGINE
Gazeti hili linazo taarifa pia kwamba vifaa katika hospitali za serikali huharibika mara kwa mara kwa sababu ya hujuma ili wagonjwa waende hospitali binafsi.
Nesi aliyejitaja kwa jina la Subi wa hospitali moja binafsi inayomilikiwa na watu wenye asili ya Bara la Asia, alisema: “Huoni siku hizi watu maskini wanakuja hapa kupima? Muhimbili, Mwananyamala na hata Amana wanawaambia waje huku.
“Daktari ambaye anamleta mgonjwa kupima huku anapata kamisheni. Vilevile tambua kwamba madaktari haohao wa hizo hospitali ndiyo hufanya hapa na kwenye hospitali nyingine binafsi kwa part-time,” alisema Subi.

SERIKALI INASEMAJE?
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, (pichani) alipoulizwa kuhusu skendo hii alijibu: “Hayo mambo siwezi kujibu sasa, labda mpaka mniandikie maswali halafu niwasiliane na vitengo vinavyohusika.”
MWANDISHI: Mheshimiwa, kuna hili hata la bei, hizi hospitali binafsi mbona zinachaji bei kubwa utafikiri kutibiwa ni anasa?
DK. MWINYI: Hilo pia siwezi kujibu, kuna vitengo vinavyohusika.
MWANDISHI: Wewe ni waziri mwenye dhamana, je, huna mpango wa kuweka sheria ya udhibiti wa bei kwenye hospitali binafsi? Mbona Ewura wanadhibiti bei za mafuta japo ni soko huria?
DK. MWINYI: Niandikie maswali halafu niletee nitashughulikia.
MWANDISHI: Na hawa Watanzania si wataendelea kupasuliwa na kutibiwa magonjwa ambayo hawaumwi kwa sababu watu wanataka pesa?
DK. MWINYI: Haya mambo yapo katika vitengo, nitayajibu kwa pamoja baada ya kunipa maswali na kuwaita wahusika.

No comments:

Post a Comment