Stori: Victor Bariety, Geita
UTATA umezidi kutanda miongozi mwa wakazi wa mji wa Geita, baada ya watu wasiojulikana kufukua kaburi kwenye makaburi ya Mtaa wa Elimu Nyantorotoro kisha kukata kichwa cha maiti iliyokuwemo na kuondoka nacho kwenda kusikojulikana usiku wa Oktoba 13, mwaka huu.
Watu
hao baada ya kufukua kaburi hilo walipasua jeneza na baadaye kutoa
kichwa cha maiti hiyo ya mwanaume ambaye utata umejitokeza kwani jina la
marehemu halijafahamika kwani waliotenda unyama huo waliondoka na
msalaba wenye jina lake na waliliacha kaburi wazi bila kulifukia.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Elimu Nyankumbu, Hassan Malima, tukio
hilo liligunduliwa saa tatu asubuhi na watu walioenda eneo hilo kuchimba
kaburi baada ya kutokea msiba kwa Mchungaji Mtafuteni Mihana wa Kanisa
la Pefa aliyefiwa na mtoto wake, Rabeka (28).
“Tulipofika
katika eneo hilo kuangalia sehemu ya kuchimba kaburi kwa ajili ya huyo
marehemu, mtoto wa mchungaji ndipo tukaona hilo kaburi likiwa
limefukuliwa,tulipolisogelea tukashuhudia maiti ikiwa imekatwa kichwa,”
alisema mwenyekiti huyo.
Uongozi wa mtaa huo baada ya kupata taarifa za tukio hilo linalohusishwa na imani za kishirikina, walitoa taarifa na polisi walifika eneo la tukio wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita, OCD Bwire.
Polisi
kwa kushirikiana na wananchi walifukua kaburi hilo na kulitoa jeneza
ili kutambua jinsia ya maiti hiyo ambapo baada ya Dk. Alex Makomba
kufanya uchunguzi iligundulika ilikuwa ya mwanaume.
Naye Mchungaji Mtafuteni alisema tukio hilo ni la imani za kishirikiana kutokana na baadhi ya wananchi kuamini kutumia njia hiyo wakiamini kuwa wanaweza kufanikiwa katika maisha yao.
“Watu
wamekosa imani ya Mungu, wanadiriki kuchukua viungo vya watu waliokufa
na kuzikwa,hivyo nawaomba watu kuachana na imani za kishirikina na
badala yake wamtegemee Mungu pekee watafanikiwa,” alisema Mchungaji
Mtafuteni.Kamanda wa Polisi mkoani Geita, ACP Leonard Paulo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Tukio hilo nina taarifa nalo na jeshi la polisi linaendelea kufanyia uchunguzi, wahusika wakipatikana watafikishwa mahakamani,” alisema.

No comments:
Post a Comment