Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, October 22, 2013

BAADA YA SUGU KUAMBIWA ANA MAPEPO HAYA NDIYO MAJIBU YAKE KWA SOPHIA SIMBA NA MARY MWANJELWA


MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA), amesema heri yeye mwenye mapepo ya ugomvi wa kupigania masilahi ya wananchi kuliko mapepo ya wizi na mipasho.
Kauli ya Mbilinyi maarufu kama Sugu imekuja siku moja baada ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba na Mbunge wa Viti Maalumu, Mary Mwanjelwa (CCM), kumshambulia kwa maneno ya kejeli jimboni kwake wakidai ana mapepo ya ugomvi.
Waziri Simba na Mwanjelwa wakiwa katika mkutano wa hadhara katika kata ya Manga, juzi, walitumia muda mwingi kumchonganisha Sugu na wananchi wake kwamba anapenda vurugu.
Akijibu hoja hizo jana kwa simu akiwa nchini China, Sugu alisema yote anayoyafanya bungeni yana baraka za wananchi wake, ambao walimtuma kupigania maslahi yao na taifa.
Alisema kazi yake si kupiga makofi na kuzomea wenzake kama wanavyofanya Simba na Mwanjelwa wanapokuwa kwenye shughuli za vikao vya Bunge.
“Nawashukuru wananchi wa Mbeya, maana baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge niliporudi nyumbani nilipokewa kwa kishindo na kunipa ruhusa ya kumkabili moja kwa moja Naibu Spika, Job Ndugai, iwapo ataendelea kuleta uhuni,” alisema.
Huku akisisitiza kauli hiyo, Sugu alisema utafika wakati atamkabili kiongozi yeyote atakayeonyesha udhaifu pale anapokalia kiti cha Spika pindi masuala muhimu ya kitaifa yatakapokuwa yanajadiliwa.
Aliwashangaa Sofia Simba na Mwanjelwa kumjadili katika jimbo lake na kuyaweka pembeni matendo yao machafu ambayo wanayafanya bungeni.
Sugu alisema mmoja wa viongozi hao anasifika kwa udokozi na wizi wa mataulo na vijiko kwenye hoteli anazofikia na kueleza kwamba hivi karibuni alisikika katika vyombo vya habari kuwa aliiba vifaa hivyo mkoani Arusha.
‘Heri mimi mwenye mapepo ya kupigania masilahi ya taifa bungeni na kama hili la juzi la muswada wa sheria, kuliko hao wenye mapepo ya udokozi na wizi wa vifaa vya hotelini.
“Matendo hayo ya udokozi ni kuliaibisha Bunge, wanawake wenzake na chama chake,” alisema.
Alisema kuwa Mbeya ni mkoa wa wacha Mungu, hivyo haiwapendezi wala hawakubaliani na mbunge ambaye anapita na kujisifu kwa matendo maovu ukiwamo uzinzi.
Sugu alimtaka Waziri Simba kutopeleka mipasho kwa wananchi wake, kwa kuwa hawajazoea mambo hayo na kumtaka kuipeleka kwa wana CCM wenzake.
Aliwataka wananchi wa Mbeya kutowasikiliza viongozi wachochezi na badala yake waendelee kupigania maendeleo yao kwa kumtuma kazi ili serikali iweze kuwajibika kwao.
“Viongozi wa CHADEMA kwao ni kupiga kazi tu, wao wasubiri mwaka 2015,” alisema Sugu.

No comments:

Post a Comment