WIMBI la matapeli wanaotumia vitambulisho vya maofisa Usalama wa
Taifa na majeshi mengine, limechukua sura mpya baada ya watu takriban
wanane, akiwamo mwanamke mmoja, kumtapeli mke wa mtoto wa Mkuu wa Wilaya
ya Ilala, Raymond Mushi, jijini Dar es Salaam.
Matapeli hao inadaiwa walisafiri kutoka Dar es Salaam hadi mjini Moshi
na kumteka mke huyo na kumsafirisha hadi jijini humo na kisha kumpora
dola za Marekani 11,000 (zaidi ya sh milioni 15).
Tukio hilo limetokea Oktoba 11, mwaka huu, eneo la Soweto mjini hapa
ambako matapeli hao wakitumia gari aina ya Toyota RAV4, walifika
nyumbani kwa mtoto wa DC huyo, Jerome Tingisi na kujitambulisha kama
maofisa wa polisi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai nchini (DCI), Robert Manumba.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Robert Boaz, watu hao walimkamata mke wa Jerome wakimtuhumu
kujihusisha na biashara ya dawa ya kulevya na kumtaka aongozane nao
hadi Dar es Salaam kwa maelezo kuwa ndiko jalada la uchunguzi
lililokofunguliwa.
Mtoa taarifa aliyeomba jina lake lisitajwe, alisema watu hao
walimchukua mke huyo na kumsafrisha hadi Dar es Salaam na baadaye
walitumia simu yake kuwasiliana na mume wake wakimtaka awape sh milioni
mbili huku wakitishia kumuua kama matakwa yao yasingetekelezwa.
Hata hivyo, mtoa taarifa wetu alisema kuwa watu hao waliamua
kumtelekeza katika eneo la Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam
huku wakiondoka na ‘breafcase’ ikiwa na kiasi hicho cha fedha.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, baada ya matapeli hao kumteka mwanamke
huyo, Hawa Jerome, walimchukua kwa maelezo kuwa wanampeleka Kituo Kikuu
cha Polisi mjini hapa lakini hawakufanya hivyo.
Jerome alithibitisha jana kutekwa kwa mkewe na licha ya kutaka habari
hizo zisichapishwe, aliongeza kuwa watekaji hao walitumia bastola, pingu
tatu na radio ya mawasiliano ya polisi kufanikisha utekaji huo.
Akizungumza na gazeti hili, Jerome alisema kuwa kwa sasa wanawasaka
watuhumiwa kwa ushirikiano na maofisa wa polisi jijini Dar es Salaam na
Moshi ili kuwatia mbaroni, huku akimtaja mmoja wao kuwa anaitwa Deo.
Alisema Deo anayeishi eneo la Kinondoni, Dar es Salaam, ndiye
aliyeongoza wenzake kumteka mkewe na amekuwa akivichafua vyombo vya dola
kwa kujipachika wadhifa wa ofisa Usalama wa Taifa, akiwa na
vitambulisho vya idara hiyo.
Hata hivyo, tukio hilo limekumbwa na habari za mkorogano, kwani
taarifa nyingine zinadai kuwa mwanamke huyo alisafirishwa hadi Dar es
Salaam na kuwekwa kwenye hoteli moja ambako aliahidi kuwapatia matapeli
hao sh milioni 100, lakini baada ya kubaini si maofisa wa polisi
aliwasiliana na jamaa yake aliyetajwa kwa jina moja la White.
|
No comments:
Post a Comment