Siku chache baada ya kuanzisha ukaguzi wa magari na watu wanaoingia katika maduka ya Mlimani City, ukaguzi huo sasa umesitishwa.
Hatua hiyo ilifuatia tishio la ugaidi baada ya
duka la Westgate la Nairobi nchini Kenya kushambuliwa na kikundi cha
Al-shabab na kusababisha mauaji ya watu 68 na wengi kujeruhiwa.
Mbali na Mlimani City lililopo Barabara ya Sam
Nujoma, jijini Dar es Salaam, maduka mengine makubwa kama vile Quality
Plaza lililopo Barabara ya Nyerere nalo lilianzisha ukaguzi kwa wateja
wake.
Hata hivyo uchunguzi wa hivi karibuni
umebainisha kuondolewa kwa ukaguzi uliokuwa ukifanywa kwa wateja na
magari yanayoingia dukani hapo, kwa madai kuwa unapunguza wateja.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina,
askari wa kike wa kampuni ya Omega Nitro inayolinda duka hilo, alisema
kuwa hatua hiyo ilikuja Oktoba 16 mwaka huu.
“Nakumbuka Jumatano baada ya kumaliza ‘shift’
niliacha ukaguzi ukiendelea, lakini niliporudi Ijumaa nikaambiwa
umesitishwa mara moja,” alisema na kuongeza:
“Kwa kweli ukaguzi wenyewe ulikuwa mgumu kwani
hatukuwa na vifaa vya kutosha na wateja ni wengi,” alisema na kuongeza:
“Katika ukaguzi tulikuta watu wengi na silaha hasa bastola wakimiliki
kihalali.”
Jitihada za kuupata uongozi wa Mlimani City
hazikufanikiwa kwa kile kilichoelezwa kuwa yuko likizo. Naye Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema hana taarifa ya
kusitishwa kwa ukaguzi, lakini akasisitiza kuwa hilo ni suala lao
binafsi.
No comments:
Post a Comment